2016-02-04 14:31:00

Warithisheni ndugu zenu imani!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi tarehe 4 Februari 2016 amesema kwamba, urithi mkubwa ambao mwamini anaweza kuwaachia wengine ni zawadi ya imani na kuwataka waamini kutoogopa kukabiliana na kifo, bali wajiandae kikamilifu, kwani mchakato wa maisha unaendelea.

Baba Mtakatifu amefanya rejea kwenye somo la kwanza ambalo Mfalme Daudi yuko kufani anaelezea kwamba, maisha yake yalikuwa yanafikia ukingoni, tayari kuungana na wazee wake katika usingizi wa mauti. Dhana ya kifo ni jambo ambalo linawaogopesha wengi, lakini huu ndio ukweli wa maisha. Waamini wanapaswa kufikiria hatua ya mwisho katika maisha yao, kwa kuuangalia mwanga wa matumaini unaopaswa kua mbele ya macho yao daima!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, siku moja wakati wa Katekesi zake za Jumatano alikutana na Mtawa wenye umri wa miaka themanini na tatu aliyekuwa na uso wa furaha, na alipokuwa anazungumza na Baba Mtakatifu alimwambia kwamba, alikuwa anakamilisha hija ya maisha yake hapa duniani, ili kuanza maisha mapya kwani alikuwa na saratani ya kongosho. Katika amani na utulivu, mtawa huyu alikuwa ameandika kurasa za maisha yake hapa duniani, tayari kuanza maisha mapya yasiyokuwa na mateso! Haya ni maneno ya matumaini.

Baba Mtakatifu anasema, Mfalme Daudi alitawala kwa muda wa miaka arobaini ambayo iliyopita kama umande wa asubuhi. Mfalme Daudi kabla ya kifo chake anamwachia Mwanaye Sulemani wosia ili kuhakikisha kwamba, anafuata sheria, amri na maagizo ya Mwenyezi Mungu. Alitambua kwamba, alikuwa ni mdhambi, lakini akawa na ujasiri wa kuomba msamaha na huruma ya Mungu. Kanisa lina mtambua kuwa ni Mtakatifu wa Mungu; mdhambi aliyetubu na kuongoka na kwa sasa alikuwa anakaribia kitanda cha mauti na hivyo anaamua kumwachia mtoto wake urithi wa imani.

Mfalme Daudi anakumbuka matendo makuu ya Mungu katika maisha yake na kumwachia kama urithi unaopaswa kutunzwa na kudumishwa. Wazazi wanapowasindikiza watoto wao kupokea Sakramenti ya Ubatizo, wanawawashia mshumaa kama urithi wa imani inayopaswa kuendelea kuwaka. Mfalme Daudi anawachangamotishwa watu kuwaachia watoto wao zawadi ya imani pamoja na ushauri mzuri. Waamini wajiulize ndani mwao ni urithi gani wanaotaka kuwaachia jirani zao. Waamini wajiandae kukabiliana na kifo bila wasi wasi kwa kujiaminisha kwa huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.