2016-02-04 15:41:00

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Kwa huruma yake kuu Mungu amekuteua, amekutakasa na anakutuma kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu “Uso wa Huruma” anatuhimiza kwamba “Huruma ni njia inayowaunganisha Mungu na binadamu, na kuufungulia moyo mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya hali yetu ya dhambi. Katika nyakati hizi tunaitwa kuitazama kwa makini sana huruma ili tuweze kuwa ishara wazi kabisa ya utendaji wa Baba katika maisha yetu”. Baba Mtakatifu anaendela kusema kwamba mwaka wa huruma unapaswa kupokelewa “kama wakati maalum kwa ajili ya Kanisa, ambapo ushuhuda wa waamini unakuwa wenye nguvu zaidi na wenye kuzaa matunda mengi zaidi”.

Masomo yote ya Dominika hi ya nne ya mwaka C wa Kanisa yanalibeba wazo hili ambapo Mungu mwenyewe anaamua kumteua mwanadamu bila kujali hali yake, anamtakasa na kumweka tayari kwa ajili ya kwenda kulitangaza neno lake. Tutafakari mambo matatu muhimu yanayojitokeza kutoka Neno la Mungu mintarafu utume wetu wa kuieneza huruma wa Mungu.

Kwanza kabisa ni uwepo wa Mungu katika utume wowote. Yeye anapaswa kuwekwa kama chanzo na kigezo cha utume wowote ule. Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuumba na anatujua nje na ndani: “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu” (Zab 139: 1 -2); Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Yeye ndiye anayejua hali zetu na mastahili yetu; Yeye ndiye anayejua anachotaka kututuma na uwezo au nguvu ya vipawa alivyotukirimia.

Somo la kwanza linatudokezea jambo lingine muhimu la kuzingatia kwa ajili ya uwepo wa Mungu katika utume wetu. Uwepo wa Mungu unatupatia utakaso: “Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa”. Kazi tunayotumwa ya kutangaza huruma ya Mungu kama tulivyosisitiza hapo juu ni kazi ya Mungu na hivyo inaashiria utakatifu. Kama tulivyokariri maneno ya Papa Francisko hapo juu kwamba “huruma ni njia inayomuunganisha Mungu na binadamu”, hali ya Mungu ya utakatifu ni ya kuzingatiwa. Hivyo uwepo wake unatia nguvu ya kuupokea utume wake katika hali ya usafi mioyoni mwetu.

Wito huu tunaoitiwa na Mungu ni kwenda kutangaza Neno la Mungu na si kazi nyingine yoyote ya kibinadamu. Mtume Petro anaambiwa katika somo la Injili “usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu”. Hii inamaanisha kwamba ufundi wake na ujasiri aliokuwa nao katika uvuvi wa samaki utatumika sasa kwa kazi ya Mungu. Mwenyezi Mungu anapotuita kwa ajili ya kazi yake Yeye ndiye anapaswa kutupangia nini cha kufanya, Yeye ndiye anayejua sababu ya wito wetu.

Kwetu wanadamu tunaoitwa tunahitajika kuvitumia vipawa alivyotujalia ili kuikamilisha kazi yake. Mtume Paulo analizungumzia hili katika somo la pili kwa namna nyingine. Kwake yeye kilicho cha msingi ni kuhubiri Injili ya Kristo kwa jinsi alivyoipokea ambaye anaielezea muhtasari wake katika fumbo zima la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Jambo la pili ambalo tunapaswa kulitafakari ni nafasi ya mwanadamu katika kuuitikia wito wa Mungu. Mtakatifu Augustino anatuambia kwamba: “Mungu aliyetuumba sisi pasipo sisi hawezi kutukomboa sisi pasipo sisi”. Hapa linasisitiziwa suala la uhuru wa mwanadamu ambalo ni haki yake msingi. Mwanadamu si kama mashine ambayo haina utashi. Yeye ni nafsi ambayo inakuwa na utayari wa kuupokea wito au sauti ya Mungu inayomjia. Hivyo, pamoja na kwamba Mungu ndiye anayetuita, Yeye ndiye chanzo cha utume wetu, nafasi yetu na hadhi yetu kama wanadamu inapaswa kuheshimiwa.

Wahusika wote wanaotajwa katika masomo ya leo wanaicheza vizuri nafasi yao ya kibinadamu na hatimaye wanakuwa tayari kuupokea utume wa Mungu. Kwanza kabisa tunaona hali ya kinadamu ya kusita kupokea wajibu kwa minajili ya udhaifu wetu kibinadamu. Mwandishi wa Kitabu cha Nabii Isaya anasema wazi kabisa: “Mimi ni mwenye midomo michafu na macho yangu yamemwona mfalme Bwana wa majeshi”. Mtume Petro anautambua ukuu Mungu na kuona hastaili kukaa mbele yake. Anadiriki hata kutaka kuifukuza huruma ya Mwenyezi Mungu: “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mweye dhambi Bwana”. Ila kwa wote huruma ya Mungu inatenda kazi na wanatakaswa na kutumwa kwenda kutangaza habari njema.

Mwanadamu katika hali ya uhuru kabisa anakubali pia kuipokea kazi ya Mungu. Utayari huu ni wa muhimu katika kuendeleza utume wetu. Sauti ya Mungu inatujia daima “nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” Mwenyezi Mungu anategemea kupokea jibu kama tunalolisikia katika somo la kwanza “Mimi hapa, nitume mimi”. Au kama Mtume Petro anavyopokea agizo la Kristo “tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki”. Kwa mara ya kwanza anaonesha hali ya kusita na wasisiwasi lakini anaitii sauti ya Mungu: “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitashusha nyavu”. Utayari wetu na ndiyo yetu kwa wito wa Mungu utuweka tayari kutekeleza kile anachotutuma tukiwa na moyo wa furaha na matumaini.

Jambo la tatu tunapaswa kutafakati ni juu ya utekelezaji wa utume wetu. Mtume Paulo anatudokezea jambo la muhimu la kuzingatia wakati wa utendaji wetu huo. Hii ni hali ya kuwa daima na Mungu kwa sababu yeye ndiye anatuita, anatutakasa na kututuma kwa kazi yake. Paulo anaitegemea daima neema ya Mungu na anasema: “na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami”. Mtume Petro anapokubali kushusha nyavu, anapokubali kutengeneza na Yesu anazaa matunda mengi. Hapa tunaonywa kwamba daima kuwa makini kuepa kishawishi cha kumwacha mwenyezi Mungu na kutenda tukiwa peke yetu katika utume wetu.

Mara nyingi tunaweza tukapitia katika nyakati za giza na zenye kukatisha tamaa. Huenda tunafikia hali hiyo sababu tunaacha kutengezena na Mungu na kuutekeleza utume wake kama vile ni kazi yetu. Hapa tukumbuke maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alipotukumbusha kwamba: “Bwana ametupatia siku nyingi za jua na upepo mwanana, siku ambazo tumevua samaki wengi; kumekuwepo na nyakati ambazo maji yalivurugwa na upepo kuwa ni wa mbisho ... lakini daima nimetambua kwamba katika mashua hiyo Bwana amekuwapo daima na daima nimetambua kwamba mashua hii, yaani Kanisa, si mali yangu, si mali yetu, ni mali yake”.

Hivyo leo hii tutafakari juu ya miito yetu. Tutambue kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayetuita na kutufanya vyombo vyake viteule ile kwenda kutangaza Neno lake kwa watu wote. Tumtegemee yeye kama nguvu yetu na kiongozi wetu ili daima tuwe tayari kulitangaza Neno lake.

Na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.