2016-02-04 14:54:00

Elimu iguse mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia elimu inayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili ili kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Baba Mtakatifu, Jumanne jioni, tarehe 3 Februari 2016 amekutana na wajumbe wa Mfuko wa Kipapa Scholas Occurentes,  mtandao wa shule ulioanzishwa nchini Argentina na Baba Mtakatifu Francisko wakati huo akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires. Lengo kuu ni kutaka kuweka uwiano bora zaidi kati michezo, sayansi na teknolojia.

Baba Mtakatifu akizungumza na wajumbe hawa amekazia umuhimu wa elimu kufumbata na kuambata utajiri wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Hizi ni tunu msingi zinazomwezesha mwanadamu kugundua utu na heshima yake inayojikita katika mapendo. Hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha utulivu na kipaji cha ugunduzi. Sanaa, michezo, tamaduni, muziki ni njia mbazo zinamsaidia mwanadamu kupata elimu na majiundo makini yanayojenga madaraja ya watu kukutana, kushirikiana na kusaidiana pasi na kuwatenga wengine katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, wao ni jeuri na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Huu ni wakati wa kujifunza na kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili, ili kuweza kuwa na maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu amesikiliza kwa makini shuhuda na miradi mbali mbali ambayo itatekelezwa na Mfuko huu wa Kipapa. Tarehe 7 Mei 2016 kutakuwa na pambano la masumbwi la kukata na shoka huko Las Vegas na tarehe 29 Mei kutafanyika pambano la amani kwenye Uwanja wa Olympic mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.