2016-02-03 14:54:00

Umuhimu wa majadiliano ya kidini katika kukuza amani duniani


Mchungaji Marcello Figueroa wa Kanisa la Kiinjili ambaye pia ni mwandishi wa habari kutoka Argentina kwa miaka ishirini na mitano amekuwa ni kiongozi wa Chama cha Biblia Argentina. Tarehe 29 Agosti 2015 alifanya mahojiano maalum na Baba Mtakatifu Francisko katika jitihada zake za kujenga madaraja ya watu kukutana ili kudumisha umoja, upendo na udugu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mchungaji  Marcelo Figueroa anasema, ameguswa kwa namna ya pekee na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video ulioandaliwa na Utume wa Sala kwa kukazia majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani ili kujenga na kuimarisha amani na maridhiano. Utume wa Sala kwa miaka mingi umekuwa ni mtandao unaosambaza nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa wakati huu, ujumbe huo kwa njia ya video umeweza kuwafikia watu wengi zaidi.

Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Francisko ametoa ujumbe wake kwa njia ya video, tarehe 6 Januari 2016 wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana. Ni ujumbe unaogusa akili na mioyo ya watu; ujumbe unaoonesha nia ya Baba Mtakatifu anayependa kuona waamini wa dini mbali mbali wakijikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Majadiliano ni tema muhimu sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.

Majadiliano ya kidini ni muhimu sana, ndiyo maana waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kusali, kutafakari, kusambaza na kuumwilisha ujumbe huu katika uhalisia wa maisha ya watu. Majadiliano ya kidini ni jambo la msingi kama alivyokazia Baba Mtakatifu wakati alipokuwa nchini Kenya, hapa hakuna mbadala. Mchakato wa kudumisha na kuimaarisha amani ni jambo ambalo linapaswa kuwakutanisha waamini wa dini mbali mbali, ili kwa pamoja kusimama kidete kukataa na kupinga vitendo vyote vinavyopelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Kuna baadhi ya waamini wanatumia jina la Mungu kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kusahau kwamba, Mungu ni upendo. Mchungaji Marcelo anasema, Baba Mtakatifu Francisko anamwelezea Mwenyezi Mungu kuwa ni Baba wa wote anayepatikana katika dini mbali mbali duniani, hali inayoonesha umoja na utofauti katika imani, lakini wote wanajitambua kwamba, ni watoto wa Mwenyezi Mungu. Kumbe, hapa majadiliano ya kidini ni muhimu sana kukuzwa na kuendelezwa badala ya kuendekeza misigano na mitafaruku ya kidini ambayo mara nyingi imekuwa ni chanzo cha mipasuko ya kijamii na mwanzo wa kutoweka kwa misingi ya haki na amani.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umewawezesha waamini na watu wengi wenye mapenzi mema kutambua  fadhila ya haki na amani ambayo Baba Mtakatifu anapenda kuipatia kipaumbele cha kwanza. Majadiliano ya kidini ni muhimu na ni dhamana ya waamini wote pasi na ubaguzi. Baba Mtakatifu alipokuwa nchini Argentina alipenda kushiriki katika majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali nchini humo, changamoto ambayo anapenda kuiendeleza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi anayeendelea kuwaalika waamini wa dini mbali mbali kuungana naye katika sala, lakini zaidi hata katika maeneo yao, kuendelea kumkumbuka na kumwombea katika sala ili aweze kutekeleza dhamana na majukumu yake kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anapowaomba waamini kusali kwa ajili yake, anaonesha kweli kwamba, anahitaji sala kutoka katika undani wa moyo wake. Papa anataka kuwaunganisha watu wa dini mbali mbali kwa njia ya sala, ili kukazia amani, yaani “Shalom” na Salam”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.