2016-02-03 11:47:00

Iweni na ujasiri wa kuandika kurasa bora zaidi za maisha ya kitawa!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameadhimisha Sherehe ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na kufunga Mwaka wa Watawa Duniani kwenye Kanisa kuu la Lubiana nchini Slovenia, Jumanne, tarehe 2 Februari 2016, kwa kuwataka watawa kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kukoleza mchakato wa kupyaisha maisha yao kiroho na kimwili, ili waweze kutekeleza dhamana na utume wao kwa moyo mweupe na wazi zaidi. Wawe na ari na moyo wa kujisadaka zaidi baada ya kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Parolin katika mahubiri yake anaendelea kukazia kwamba, Mwenyezi Mungu ameonesha uwepo wake wa karibu na binadamu dhaifu na mdhambi kwa njia ya wito na maisha yao ya kitawa. Hii ni historia inayopaswa kukumbukwa na kuendelezwa daima kwa kujikita katika udugu na adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu. Watawa wawe mstari wa mbele kuendeleza kazi za kimissionari zilizotekelezwa na wamissionari kwa nyakati mbali mbali kwa kuendeleza Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda na huduma makini katika sekta ya elimu na utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Watawa waguswe na mahangaiko ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, daima wakiendeleza mchakato wa maboresho ya maisha ya kitawa mintarafu changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Historia ya maisha yao inasheheni utajiri mkubwa wa shuhuda za maisha, mwaliko kwa watawa kuwa kweli ni watu wa shukrani na wanaowajibika barabara kutokana na urithi waliojaliwa kuupata. Wawe na ujasiri wa kujenga kesho iliyo bora zaidi, huku wakimtumainia Roho Mtakatifu anayetaka wafanye mambo makubwa zaidi.

Kardinali Parolin anawakumbusha watawa kwamba, mbele yao pia kuna changamoto ya kupungua kwa idadi ya miito ya kitawa na kazi za kitume. Kuna idadi kubwa ya wazee, changamoto za kiuchumi na kijamii, hasa baada ya myumbo wa uchumi kimataifa; changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; fikira za mawazo mepesi mepesi, ubaguzi bila kusahau changamoto za kijamii, kama ambavyo anafafanua Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Watawa wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Pamoja na changamoto zote hizi, watawa wanapaswa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Mzee Simeoni na Nabii Anna wanashuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha ya Mtoto Yesu ambaye atakuwa kweli ni wokovu wa watu wake na nuru ya mataifa. Watawa wawe na matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu atawajalia neema na baraka za kuendelea kuandika kurasa za historia ya maisha ya kitawa hata kwa siku za usoni, jambo la msingi kwa watawa ni kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha. Wawe makini kwa mambo msingi na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Watawa wajenge mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakari na Sakramenti za Kanisa; huku wakijitahidi kumwilisha mashauri ya Kiinjili katika maisha yao yao ya kila siku. Watawa wawe ni Mahekalu Matakatifu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, daima wakikimbilia tunza na ulinzi kutoka kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.