2016-02-02 11:44:00

Wanaume na wanawake washirikiane kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu


Watu wakiangalia kwa haraka haraka picha ya Kanisa inayowasilishwa na vyombo vya mawasiliano ya kijamii ni ile inayowaonesha wanaume wakiwa mstari wa mbele katika ujenzi wa Kanisa. Picha hii inaweza kuonekana kwenye Ibada, mikutano na matukio mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa. Lakini ikumbukwe kwamba, wanawake wamekuwa  mstari wa mbele kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Hawa ni wanawake wa shoka waliojifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa; Mama wa huruma na upendo wa Mungu; Mama wa Msamaha, neema na furaha takatifu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wanawake wameendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Kanisa hata katika ukimya wao.

Mtakatifu Paola alikuwa ni mwanamke wa shoka aliyeshirikiana na Mtakatifu Jerome kuandika tafsiri ya Biblia kwa lugha ya Kilatini, maarufu kama Vulgata. Huu ukawa ni mwanzo wa Mapokeo makubwa ya Kitaalimungu kwa Kanisa la Mashariki. Hata katika Agano la Kale kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya wanawake wenye imani na Mababa wa Imani. Wanawake wameendelea kuchangia hata katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa mfano kumekuwepo na ushirikiano wa karibu sana kati ya mwana taalilimungu Hans Urs Von Baltasar na Mama Adrienne von Speyr, daktari na mtaalam wa maisha ya kiroho. Ushirikiano wao umekuwa ni mwanzo wa machapisho muhimu yenye mwelekeo mpya katika maisha ya kiroho.

Bila shaka watu wengi wanamkumbuka Mama Chiara Lubich, mwanamke wa kwanza katika historia na maisha ya Kanisa kuanzisha Chama cha Kitume cha Wafokolari, kinachowashirikisha wanawake na wanaume katika ujenzi wa maisha ya na utume wa Kanisa katika sekta mbali mbali. Tofauti kati ya wanawake na wanaume ni utajiri mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa na kielelezo makini cha sauti ya kinabii. Kumbe kuna haja kwa wanawake na wanaume kushirikiana kwa pamoja katika maisha na utume wa Kanisa ili kushuhudia huruma na upendo wa Mungu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa ufalme wa Mungu hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.