2016-02-02 08:57:00

Mashuhuda wa Mfufuka!


Zaidi ya Maaskofu 1, 500 tangu mwaka 2001 wamehudhuria kozi maalum zilizokuwa zinaandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki pamoja na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, ili kuwasaidia Maaskofu kutekeleza vyema dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika Makanisa mahalia.

Kozi hizi pia zimekuwa ni fursa kwa Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kufahamiana, kujenga na kudumisha umoja na udugu katika urika wao; kwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Sekretarieti ya Vatican na hatimaye, Baba Mtakatifu mwenyewe anayewateua na kuwatuma ili kuchunguza Kondoo wa Kristo. Haya yamesemwa na Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu, Jumatatu tarehe Mosi Februari 2016 wakati wa kuzindua kitabu ambacho ni mkusanyiko wa semina zilizotolewa kwa Maaskofu katika kipindi cha mwaka 2015, kinachojulikana kama “Mashuhuda wa Mfufuka”, kitabu ambacho kimechapishwa na Idara ya Uchapaji ya Vatican, LEV.

Uzinduzi wa Kitabu hiki umeratibiwa na Bwana Greg Burke, Msemaji mkuu msaidizi wa Vatican ambaye, tarehe Mosi Februari 2016 ameanza kazi rasmi baada ya Padre Ciro Benedettini, kung’atuka kutoka madarakani baada ya kutumikia Ofisi ya Habari ya Vatican kwa takribani miaka ishirini na kutoa huduma iliyotukuka. Tukio hili limehudhuriwa pia na Askofu mkuu Ilson Jesus Montanari, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu pamoja na Askofu mkuu Francesco Cacucci wa Jimbo kuu la Bari-Bitondo.

Kardinali Marc Ouellet anakaza kusema, licha ya Sakramenti ya Daraja Takatifu kumkirimia Askofu neema na baraka katika utekelezaji wa dhamana na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, bado Askofu anapaswa kujichimbia katika vitabu ili kuendelea kunoa akili yake; kusali, kutafakari pamoja na kusoma alama za nyakati kwa kuangalia mabadiliko yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Katika mwelekeo huu, Maaskofu ambao wamekwishatimiza miaka mitano ya huduma, watakuwa pia wanaalikwa ili kuendelea kujipyaisha katika maisha na utume wao ili kamwe wasipitwe na wakati. Huu ni mchakato wa malezi na majiundo endelevu kwa Maaskofu. Kama sehemu ya mchakato wa majiundo endelevu, kuna haja kwa Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kukutana pamoja, ili kushirikishana na kutajirishana furaha, fursa, matumaini, shida na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao kama wachungaji wakuu. Roma ni mahali muafaka pa Maaskofu kukutana kwani hapa ni kitovu cha Kanisa Katoliki.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Montanari anasema, kwa miaka yote hii, hizi kozi zimechambua tema mbali mbali kuhusu: Uongozi wa Kanisa, Shughuli za Kichungaji: Dhamana ya Askofu katika kuongoza, kufundisha na kutakatifuza watu wa Mungu. Mambo yote haya yameingizwa katika Kitabu hiki pamoja na hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani. Maelezo yote haya yanafafanua kwa kina na mapana mwelekeo wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Maaskofu wa Kanisa Katoliki.

Naye Askofu mkuu Cacucci ambaye amekuwa ni kati ya wawezeshaji wakuu anasema, baadhi ya tema zimewasaidia Maaskofu kutambua umuhimu wa kuzingatia mambo makuu katika maisha ili kuwasaidia wakleri kuweza kutafuta na hatimaye, kuambata mambo msingi katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Askofu anapaswa kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wake kama mchungaji mkuu wa kundi lake. Awe ni kiongozi anayewapenda na kuwaheshimu Wakleri wake kwani hawa ni wasaidizi wake wa kwanza katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.