2016-02-02 14:38:00

Kanisa linahitaji vijana watakaojitosa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Injili ya furaha Evangelii gaudium, anasema, familia ya mungu inawajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa ushuhuda unaojikita katika imani tendaji. Huu ni mwaliko wa kumwilisha imani katika tamaduni za watu kwa kujikita katika mchakato wa utamadunisho.

Wakristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki kikamilifu: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo, hivyo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa. Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili anasema Padre Dietrich Pendawazima, Makamu mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Consolata katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Mahitaji ya kimissionari ni makubwa sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, bado kuna haja ya kukuza na kudumisha miito ya kitawa na kipadre, ili Kanisa liweze kupata watendakazi watakatifu, wema na waadilifu watakaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za dunia. Wamissionari wa Consolata wanaendelea kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Daima wanamshukuru Mungu kuona kuna vijana wanaojitosa na kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa; tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano. Mwaka wa Watawa Duniani, imekuwa ni nafasi ya kusali kwa ajili ya kuombea miito, kuimarisha na kukuza zaidi wito wa maisha ya kitawa. Wamissionari wa Consolata wanaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili awajalie vijana wengi, wema na watakatifu watakaothubutu kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na huruma ya Mungu kwa waja wake! Anasema Padre Pendawazima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.