2016-02-01 07:59:00

Utajiri wa nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha ya kiroho!


Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa anasema, wakati wa Kipindi cha Majilio, katika Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuhitimishwa kwa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, katika tafakari zake kwa Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu alichambua kwa kina na mapana: Nyaraka za Mwanga wa Mataifa, “Lumen Gentium”. Wakati wa Kwaresima kwa mwaka 2016 atajika zaidi katika Tamko la Liturujia “Sacrosanctum Concilium” , Neno la Mungu “Dei Verbum”, Kanisa katika Ulimwengu Mamboleo “Gaudium et spes" na Majadiliano ya kiekumene “Unitatis redintegratio”.

Lengo ni kupitia nyaraka hizi za Kanisa katika mwanga wa maisha ya kiroho. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican umeleta mwamko na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kanisa, kumbe tafakari hizi zitasaidia kuangalia matunda ambayo yamejitokeza ndani ya Kanisa katika kipindi cha miaka 50 tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulipoadhimishwa. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kumbu kumbu ya hitimisho la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni changamoto ya kufanya tafakari ya kina ili kuangalia hija ambayo Mama Kanisa ameifanya katika maisha ya kiroho kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Itakumbukwa kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni mchakato ambao umeliwezesha Kanisa kukutana na kujadiliana na watu wa nyakati hizi. Ni changamoto ambayo Roho Mtakatifu amelipatia Kanisa ili kutoka huko lilikojichimbia, tayari kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu kwa kujikita katika ari na mwamko mpya wa kimissionari, ili kukutana na watu mahali na katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Mama Kanisa anatumwa kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya furaha, kwa kumwilisha huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu. Waamini katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu waoneshe ari na mwamko huu wa kimissionari unaojikita katika ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma.

Hiki ni kipindi muafaka cha kuhakikisha kwamba, Kanisa linaonesha ujasiri wa Msamaria mwema kama alivyokazia Mwenyeheri Paulo VI alipokuwa anahitimisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waamini wanapopita kwenye Lango la Huruma ya Mungu, wanahimizwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, kielelezo cha Msamaria mwema. Nataka rehema na wala si sadaka” (Mt. 9:13) ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Padre Cantalamessa atatoa tafakari za Kwaresima kwenye Kikanisa cha “Redemptoris Mater”  saa 3:00 asubuhi kila Ijumaa kama ifuatavyo: Tarehe 19 na 26 Februari 2016; baadaye tarehe 4, 11, 18 Marchi 2016. Hiki ni kipindi muhimu cha kujichotea utajiri unaofumbatwa kwenye Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha ya kiroho, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.