2016-01-31 09:10:00

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa kuadhimishwa 2020 Budapest!


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 31 Januari 2016 ametuma ujumbe kwa njia ya Video kwa washiriki wa Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa linaloongozwa na kauli mbiu“Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu” huko Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini. Baba Mtakatifu anakumbuka hija yake ya kitume nchini Ufilippini, mwaka mmoja uliopita, wakati ambapo watu wengi nchini Ufilippini walikuwa wameathirika kutokana na dhoruba ya Yolanda, huko akashuhudia imani thabiti ya familia ya Mungu, zawadi waliyoipokea takribani miaka 500 iliyopita chini ya usimamizi wa Mtakatifu Nino.

Waamini nchini Ufilippini wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kutokana na uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake. Wamekuwa ni wamissionari wanaoendelea kusambaza mwanga wa Injili Barani Asia hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kamba, kauli mbiu ya maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa inawakumbusha waamini kwamba, Kristo Mfufuka daima yuko pamoja na Kanisa lake, lakini kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake Azizi. Uwepo huu si tu faraja, bali pia na ahadi na mwaliko.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni ahadi ya furaha na amani ya kweli itakayotawala kwa wakati wa utimilifu wa nyakati. Huu ni mwaliko wa kusonga mbele kama Wamissionari ili kutangaza na kushuhudia ujumbe wa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na msamaha kwa kila binadamu. Ujumbe huu ndiyo kiu ya walimwengu kwa wakati huu, kutokana na uwepo wa vita, ukosefu wa haki sanjari na mipasuko ya kijami. Wakristo wanapaswa kuwa ni wamissionari na wafuasi amini wa Kristo, ili kuwatangazia watu Habari Njema ya upendo unaokoa, upatanisho, haki na amani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kongamano hili limeadhimishwa katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kuwawezesha waamini kuingia katika kiini cha Injili yaani huruma inayopaswa kusambazwa kwa familia ya Mungu; ili kuganga na kuponya madonda; kuwapatia watu matumaini wale waliokata tamaa. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kutafakari kwa kina na mapana Ekaristi Takatifu mintarafu ari na mwamko wa kimissionari, unaojionesha katika huduma kama Yesu mwenyewe alivyofanya kwa kuwaosha mitume wake miguu.

Yesu katika maisha na utume wake alitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wadhambi na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Akajitaabisha kuwasikiliza na hatimaye, akawaonjesha huruma na upendo wa Baba yake wa mbinguni. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yawe ni changamoto ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo, kwa kuheshimiana na kuwa wazi ili kuwapokea na kuwahudumia jirani.

Kanisa Barani Asia, linaendelea kujikita katika majadiliano ya kidini kama kielelezo cha ushuhuda wa kinabii unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Kwa njia ya ushuhuda, upendo wa Mungu unakuwa ni chachu ya mageuzi katika maisha ya watu na kwa njia hii, inakuwa ni rahisi zaidi kutangaza upatanisho, haki na umoja wa familia ya binadamu. Ushuhuda wa maisha unaweza kusaidia kufunua mioyo ya watu kwa Roho Mtakatifu kiasi hata cha kumfuasa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Yesu aliwaosha miguu mitume wake, kielelezo cha unyenyekevu na huduma ya mapendo, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake pale juu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ekaristi Takatifu ni shule ya huduma ya unyenyekevu, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine; kiini cha umissionari na ufuasi wa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Ufilippini ambao daima wamekuwa mstari wa mbele kuonesha mshikamano, upendo na wema. Watu wanapania daima kujenga si nyumba tu, bali maisha yao, kielelezo cha nguvu ya Ekaristi Takatifu inayopyaisha maisha na kubadili mioyo ya waamini, tayari kuwahudumia na kuwalinda maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mwaliko wa kujitahidi kuwa wakamiliifu kwa kukataa ukosefu wa haki, rushwa na ufisadi; mambo yanayotia sumu mizizi ya kijami.

Baba Mtakatifu Francisko anawatakia wajumbe wote imani thabiti na upendo kwa Kristo anaendelea kuwepo katika Ekaristi Takatifu, ili kweli waweze kuwa ni Wamissionari na wafuasi amini wa Kristo; kwa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa sanjari na kuendeleza ari na mwamko wa kimissionari katika Makanisa mahalia. Ekaristi Takatifu iwe ni chachu ya upatanisho na amani duniani kote.Baba Mtakatifu anatangaza kwamba, Maadhimisho ya Kongamanio la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, litaadhimishwa Budapest, Hungaria, kunako mwaka 2020. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga pamoja naye katika sala, ili kuombea maandalizi na hatimaye mafanikio katika maadhimisho ya Kongamano hilo. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume akiwaombea furaha na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.