2016-01-31 13:56:00

Huruma ya Mungu haiwezi kuwekewa kizingiti na mtu awaye yote!


Yesu baada ya kuanza maisha yake ya hadhara alirejea kijijini Nazareti na hapo akasoma sehemu ya Maandiko Matakatifu kwa kuwaelezea kwamba, utabiri uliotolewa na Nabii Isaya katika Agano la Kale sasa unapata utimilifu wake. Watu wanamshangaa na kuanza kunong’onezana kati yao juu ya wasifu wa Yesu, huku wakimtaka atende miujiza ambayo wamesikia kwamba, Yesu alitenda huko Kapernaumu. Lakini kwa bahati mbaya Yesu hakutenda muujiza kwani anasema, Nabii hakosi heshima isipokuwa kwa watu wa nyumbani kwake.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 31 Januari 2016 kwa waamini waliokuwa wamefuruka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Yesu katika mahubiri yake amewataja pia Manabii wakuu: Eliya na Elisha waliofanya miujiza kwa wapagani kutokana na ugumu wa mioyo ya watu wao. Maneno haya anasema Baba Mtakatifu yalitibua nyongo ya watu, nao wakajaa ghadhabu, wakaondoka, wakamshika na kumtoa nje ili wapate kumtupa chini, ili akione cha mtema kuni, lakini Yesu akapita kati kati yao na kwenda zake, kwani Saa yake ilikuwa bado haitatimia.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwinjili Luka anaweka mbele ya macho ya wasomaji wake kishawishi ambacho waamini wanapaswa kukikwepa kwa kudhani kwamba, dini ni dhamana ya uwekezaji unaofanywa na binadamu, kiasi cha kumtumia Mungu ili kufanikisha mafao binafsi. Kumbe, hapa changamoto ni kukubali kupokea mwaliko wa ufunuo wa Mungu unaomwonesha Mwenyezi Mungu kuwa ni Baba anayewajali viumbe wake, hata wale wanaonekana kutokuwa na thamani kubwa mbele ya macho ya binadamu. Hakuna sababu yoyote ya kibinadamu inayoweza kuwa ni kikwazo cha mtu kutengwa na huruma ya Mungu, kila mtu anaupendeleo wa pekee wa kujiachia mikononi mwa Mungu.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Neno la Mungu linaendelea kutangazwa kila siku kwa ajili ya wokovu wa binadamu, unaonesha kwamba, Mungu anataka kukutana na watu wake katika hali na mazingira yao kama anavyofanya kwa wakati huu. Mwenyezi Mungu ndiye wa kwanza kuchukua hatua, ili kuwatembelea na kuwaonjesha waja wake huruma, kwa kuwainua kutoka katika mavumbi ya dhambi na kuwaketisha mahali pa juu kabisa, ili kuangusha kiburi na majivuno ya binadamu.

Mwenyezi Mungu anawataka watu wake kupokea ukweli unaofariji kutoka katika Injili, ili kutembea katika njia ya wema na utakatifu wa maisha. Bikira Maria alikuwepo na kushuhudia Mwanaye wa pekee akitishiwa kifo, Yesu ambaye alishangiliwa kwa mara ya kwanza, leo anatishiwa kifo. Bikira Maria akiwa amejaa imani thabiti, aliyaweka yote haya moyoni mwake, awasaidie waamini kutubu na kumwongokea Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.