2016-01-30 07:16:00

Wamissionari 1071 wa Huruma ya Mungu kutumwa duniani kuwaondolea watu dhambi


Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjili mpya anasema, tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kumekuwepo na idadi kubwa ya waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaofanya hija kila siku kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ili kuomba huruma ya Mungu. Hadi wakati huu, kuna idadi ya mahujaji kutoka: Kenya, Msumbiji na Pwani ya Pembe wamehudhuria kwa upande wa Bara la Afrika.

Maadhimisho haya yanaendelea kugusa akili na nyoyo za watu kwa namna mbali mbali, ili kuwasaidia waamini kutambua, kuonja na kuwamegea wengine huruma na upendo wa Mungu unaojifunua katika kila siku ya maisha ya mwanadamu. Kumekuwepo na ushiriki mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hali inaoonesha kwamba, wengi wa maguswa na mchakato wa maadhimisho, kielelezo makini kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amesoma alama za nyakati na kujitahidi kuzima kiu ya matarajio ya watu wa Mungu kwa nyakati hizi.

Ingawa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanafanyika sehemu mbali mbali za dunia, lakini bado Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican lina nafasi na umuhimu wake wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kupita katika Lango la Huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Katika maadhimisho haya, hapo tarehe 3 Februari 2016, Masalia ya Mtakatifu Leopoldo Mandic na Mtakatifu Padre Pio wa Pietracina yatawasili mjini Roma na kupokelewa kwenye Kanisa la Mtakatifu Lorenzo, nje ya kuta za Roma. Hawa ni watakatifu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Tarehe 5 Februari 2016 majira ya jioni, kutakuwepo na maandamano kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Masalia haya yatabaki kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hadi tarehe 11 Februari 2016, baada ya Misa ya shukrani, Masalia haya yatarejeshwa tena sehemu zake.

Tarehe 10 Februari 2016 Jumatano ya Majivu, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, Baba Mtakatifu Francisko atawatuma Wamissionari 1071 wa Huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao kuna Wamissionari mia saba ni kutoka: Tanzania, Burundi na Zimbabwe kwa upande wa Bara la Afrika. Wamissionari hawa watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 9 Februari 2016 ili kuonesha umuhimu na utajiri wa Fumbo hili la imani. Hawa ni Mapadre watakaopewa mamlaka ya kuwaondolea waamini dhambi ambazo kimsingi zinaondolewa na Kiti cha kitume.

Lengo ni kuwaonjesha msamaha wale wote wanaotaka kukimbilia huruma ya Mungu, kwa kumkazia macho Yesu, Kuhani mkuu mwenye rehema na mwaminifu katika mambo ya Mungu. Wamissionari kumi wataadhimisha Ibada pamoja na Baba Mtakatifu Francisko na hapo watapokea mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi zao. Kwa ufupi haya ndiyo ambayo yanaendelea kujiri katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ndani na nje ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.