2016-01-30 14:49:00

Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Maboresho ya huduma za Afya


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kutokana na mamlaka aliyokabidhiwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 14 Januari 2016, kwa kuzingatia mahitaji ya uanzishwaji wa Tume ya Kipapa ya huduma za kichungaji katika sekta ya afya kwa viongozi wenye dhamana na Kanisa amemteua Monsinyo Luigi Mistò, Katibu mkuu wa Idara ya Uongozi katika masuala ya kiuchumi ambaye pia ni Rais wa Mfuko wa Hifadhi ya Afya mjini Vatican, FAS kuwa Rais wa Tume hii mpya na katibu wake atakuwa Sr. M. Annunziata Remosso, O.M.V.F. Afisa kutoka Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume. Kwa sasa Tume hii itajikita zaidi katika shughuli zake nchini Italia.

Wengine walioteuliwa ni pamoja na:

Monsinyo Carmine Arice, Kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Prof. Carlo Cardia, kutoka Chuo Kikuu cha Roma Tre.

Dr. Mariella Enoc, Rais wa Baraza la Uongozi wa Hospitali ya Bambino Gesù.

Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu, Katibu mkuu Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya.

Dr. Enrico Zampedri, Mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Agostino Gemelli.

Wajumbe hawa watatekeleza dhamana hii kwa muda wa miaka mitatu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anawataka wajumbe kuchangia kadiri wanavyoweza katika mchakato wa maboresho ya shughuli na huduma zinazotolewa na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kwa kuzingatia karama na moyo wa waanzilishi wa Mashirika husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.