2016-01-30 08:08:00

Ushuhuda wa Injili ya furaha ni dhamana nyeti kwa maisha na utume wa watawa!


Hitimisho la Maadhimisho ya Mwaka  wa Watawa Duniani, limeanza kwa mkesha wa sala na tafakari; kwa makongamano na semina; kwa hija na ibada mbali mbali, ili kuwawezesha watawa kutambua na kuthamini maisha na utume wao ndani ya Kanisa, kwamba, wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya furaha na huruma ya Mungu kwa binadamu. Maisha ya kitawa yanajikita katika umoja unaojionesha katika tofauti mbali mbali za maisha na karama. Watawa wanahamasishwa anasema Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume wakati wa tafakari yake kwenye mkesha wa sala ya kufunga Mwaka wa Watawa Duniani.

Dhamana ya Watawa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha ni jambo ambalo halina mbadala, kwani hii ni sehemu ya maisha na vinasaba vya utume wao kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Wao ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu, mwaliko kwa watawa kutekeleza dhamana hii pasi na mzaha. Wawe na ujasiri wa kutoka kimasomaso ili kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu na kuondokana na kishawishi cha kutaka kujitafuta na kujifungia katika viota vyao wenyewe!

Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume anasema, watawa wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya furaha inayokata kiu ya maisha ya mwanadamu, kwa kujikita katika umoja na udugu; kwa kuendelea kumwilisha karama na tasaufi za mashirika yao katika mshikamano wa upendo na Kanisa zima. Watawa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na watu, kuwasikiliza kwa makini na kuwahudumia kwa ari na moyo mkuu, changamoto ambayo imetolewa na Padre Christoph Theobald, SJ.,

Siri ya umoja na utofauti unaofumbatwa katika maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa ni uwepo endelevu wa Mungu anayetenda kazi na watu wake katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Hapa watawa wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na kufunga kama njia ya kuratibu vilema na mapungufu yao ya kibinadamu.

Watawa wajitahidi kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo, katika tafakari na huduma; kwa kuonesha upendo, upole, huruma na unyenyekevu kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha yake. Haya ni mambo msingi yanayoshuhudia Injili ya furaha na huruma ya Mungu katika maisha na utume wa watawa. Roho Mtakatifu anaendelea bado kutenda kazi ndani ya Kanisa kwa kuamsha mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume. 

Watawa watambue kwamba, maisha na utume wao ni maabara ya maisha ya Kanisa, mwaliko wa kushuhudia Injili ya furaha iliyoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Watawa wawe na ujasiri wa kuanzisha nyumba zinazojikita hata katika majadiliano ya kiekumene, kwa kushirikishana karama na watawa wa Makanisa mengine duniani na kwa njia hii, Kanisa litaendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika: sala, huduma, ukweli na ushuhuda wa damu ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Watawa wasaidie kuhamasisha dhamana, nafasi na utume wa wanawake katika maisha ya Kanisa.

Kwa upande wake, Sr. Maria Ignazia Angelini, OSB amekazia umuhimu wa tafakari kuwa ni sehemu na mtindo wa maisha kwa watawa; mambo yanayomwilishwa katika huduma na ufuasi kwa Kristo Yesu aliyejitoa sadaka kielelezo cha utii, ufukara na useja. Kanisa lina utajiri mkubwa wa watawa waliojipambanua katika tafakari ya kina iliyomwilishwa katika huduma kwa Mungu na binadamu. Hawa ni Mtakatifu Yohane wa Msalaba, Mama Theresa wa Calcutta na Mtakatifu Carlo Carretto; wote hawa wamekuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha. Kumbe, watawa wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa tunu hizi katika maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.