2016-01-29 12:14:00

UN na Benki ya Dunia kushirikiana katika kukabiliana na tatizo la maji!


Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani uliokuwa unafanyika huko Davos, Uswiss umekuwa ni fursa kwa wafanyabiashara wa kimataifa, viongozi wa Jumuiya na Mashirika ya Kimataifa kuangalia kwa pamoja changamoto zinazomkabili mwanadamu katika medani mbali mbali za maisha, ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu, aliwaomba kamwe wasiwasahau maskini katika sera, mikakati na vipaumbele vyao.

Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia wanatambua kwamba, maji ni kati ya changamoto kubwa inayiandama familia ya binadamu. Taasisi hizi zimeanza kufanya mchakato wa kuunda kikosi kazi kitakachoshughulikia tatizo na changamoto ya maji na huduma ya afya. Maamuzi haya yamefikiwa wakati ambapo nchi nyingi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama; wakati huo huo kuna nchi ambazo zinaendelea kuandamwa na athari za mafuriko. Changamoto ya maji ni kwa dunia nzima na wala si tu kwa nchi maskini kama ambavyo wengi wanashawishika kufikiri.

Baadhi mbaya kuna baadhi ya watu wanatumia maji ambayo si safi wala salama kwa matumizi ya binadamu, hali ambayo inahatisha maisha, ustawi na maendeleo ya watu hawa. Ili kuboresha maisha ya watu, kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati utakaowawezesha watu wengi kupata maji safi na salama pamoja na kudhibiti athari zinazotokana na mabadiliko ya tabiabchi, changamoto ambayo imetafutiwa ufumbuzi hivi karibuni katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi uliohitimishwa hivi karibuni huko Paris, Ufaransa.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna kiasi cha watu billioni moja na millioni laki tatu ambao hawana uhakika wa maji safi na salama. Kila mwaka watu millioni tatu wanalazimika kunywa maji yaliyocheshwa au yaliyotekwa kwenye mabwawa au mito yenye maji yaliochafuriwa kutokana na matumizi ya binadamu, hali ambayo inapelekea watu wengi kupatwa na magonjwa na hatimaye kufariki dunia.

Matumizi mabaya ya maji, uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote na uharibifu wa ekolojia ni mambo ambayo yamesababisha kupungua kwa upatikanaji wa maji safi na salama. Wataalam wa masuala ya maji wanakaza kusema, ifikapo mwaka 2025, upungufu wa maji safi na salama utakuwa umefikia asilimia 56% duniani kote. Ikumbukwe kwamba, maji ni uhai, yanapaswa kutunzwa kwa heshima na nidhamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.