2016-01-29 06:28:00

Kongamano la Ekaristi Takatifu chachu ya majadiliano ya kidini!


Askofu mkuu Thomas Menamparampil, wa Jimbo kuu la Guwahati, India ambaye ni kati ya wawezeshaji wakuu katika maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa lililofunguliwa tarehe 25 Januari 2016 huko Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini anasema kongamano hili ni chachu muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kidini Barani Asia, ili kushuhudia tunu msingi za Injili kwa kujikita katika haki, amani na maridhiano. Ni kipindi cha sala na tafakari ya kina, hasa wakati wa kuabudu Ekaristi Takatifu, kwani hapa waamini wanakutana na kuzungumza na Yesu Kristo, huruma ya Baba wa mbinguni.

Kanisa Barani Asia linapaswa kumwilisha Injili ya Kristo kwa kumfuasa Kristo aliyejisadaka hadi kuyamimina maisha yake ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa Familia ya Mungu kujitosa na kujisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali, ili waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao. Hapa waamini wanapaswa kusikiliza kilio cha Yesu kinachoendelea kusikika kati ya watu wanaoteseka ndani na nje ya Bara la Asia.

Majadiliano ya kidini ni chachu ya umoja, upendo na mshikamano wa kidugu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, tofauti zao za kidini ni utajiri mkubwa kwa binadamu wote. Lengo ni kukuza majiundo ya pamoja, ushirikiano na mshikamano katika nyanja mbali mbali za maisha. Mshikamano huu unaweza kujikita kwa namna ya pekee kwa kuthamini na kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimataduni.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kama njia mahususi ya kupambana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha ya mwanadamu. Kwa namna ya pekee, waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Waamini wawe ni mashuhuda wa kanuni maadili katika shughuli mbali mbali wanazotenda katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na maendeleo ya jamii, pasi na maadili, mchakato wa Uinjilishaji utagonga mwamba! Uinjilishaji hauna budi pia kwenda sanjari na utamadunisho, ili imani iweze kuingia na kuzama katika akili na mioyo ya watu, ili kusafisha na kuondoa mambo yote yanayosigana na tunu msingi za Kiinjili, tayari kuambata na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini watambue tunu msingi za tamaduni na mapokeo yao, tayari kuzipatia nafasi katika ushuhuda wa imani, wawe na ujasiri wa kuondokana na mila, tamaduni na desturi zinazosigana na Injili.

Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta ambaye anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu wakati wowote kuanzia sasa awe ni mfano bora wa Uinjilishaji mpya unaoongozwa na Injili ya huruma ya Mungu inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, mafao, ustawi na maendeleo ya binadamu wote: kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini ya kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu kwa matendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.