2016-01-27 07:11:00

Kwaresima ya Jubilei ya huruma ya Mungu: upendo na huruma ni chanda na pete!


Nataka rehema na wala si sadaka (Mt. 9:13) ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambayo kwa mwaka huu inaanza Jumatano ya majivu hapo tarehe 10 Februari 2016, kwa mwaliko wa kutubu, kusali, kuongoka, kutafakari pamoja na kujikita katika matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kwaresima ya Jubilei ya huruma ya Mungu umewasilishwa kwa waandishi wa habari, Jumanne tarehe 26 Januari 2016 na Kardinali Francesco Montenegro, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Agrigento, Italia pamoja na Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki Cor Unum pamoja na Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu msaidizi wa Cor Unum.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu wakati wa Kipindi cha Kwaresima unalenga kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukiishi kipindi hiki maalum katika maisha ya Wakristo kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Kardinali Montenegro katika tafakati yake, amejikita katika mambo makuu matatu: huruma ya Mungu mintarafu Maandiko Matakatifu; umuhimu wa matendo ya huruma na mwishoni, Kwaresima na hija ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Montenegro anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu anakazia umuhimu wa huruma ya Mungu kama kielelezo cha ufunuo wa Mungu unaopata hitimisho lake kwenye Fumbo la Msalaba, pale Yesu anapoonesha mikono ya huruma inayosamehe. Kwaresima kiwe ni kipindi ambacho kitawasaidia waamini kujikita katika kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao.

Iwe ni fursa ya kuonja huruma ya Mungu kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujipatanaisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Kwa namna ya pekee, Kwaresima ya Mwaka huu iwe ni nafasi ya kujikita pia katika kukuza, kudumisha haki na amani. Huruma ya Mungu iwe ni chachu inayoleta mabadiliko katika maisha ya waamini, ili kwa kuwa waaminifu, waweze pia kuwaonjesha jirani zao huruma ya Mungu.

Kardinali Montenegro anasema, Kwaresima ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuutafakari kwa makini Uso wa huruma ya Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini wa hali na kipato. Matendo ya huruma anasema Baba Mtakatifu Francisko yanawawezesha waamini: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu; kuwavika walio uchi; kuwakaribisha wageni; kutembelea wagonjwa; kutembelea wafungwa pamoja na kuzika wafu. Matendo huruma kiroho anakaza kusema Baba Mtakatifu ni kuwapatia ushauri wenye mashaka; kuwafundisha wajinga; kuwaonja wakosefu; kuwafariji wenye huzuni; kusamehe makosa; kuwavumilia wasumbufu, kuwaombea wazima na wafu, ili wote hawa waweze kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao.

Mambo yote haya anakaza kusema Kardinali Montenegro yanagusa undani ya maisha ya mwamini ambaye anaogelea katika lindi la dhambi na mauti. Waamini wanaalikwa na Baba Mtakatifu kujipatia chakula cha Neno la Mungu wakati wa Kwaresima, ili kulimwisha Neno hili kama ushuhuda wa imani tendaji katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wanakumbushwa kwamba, watahukumiwa kadiri ya matendo ya huruma kwa jirani zao, kumbe hapa kuna haja ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Waamini wajitahidi kuwa na dhamiri nyofu.

Kwaresima ya Mwaka huu inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwamba, Fumbo la Pasaka ni kiini cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hapa waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho, kwa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya jirani. Sura ya Lazaro maskini, iwe ni mwaliko wa kuwaonjesha wengine upendo na huruma ya Mungu. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kusikiliza kilio cha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini wanapopita katika Malango ya Huruma ya Mungu, wawe tayari kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Kwaresima iwe ni fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu; fursa ya Kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu; wakati uliokubalika wa kutekeleza matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa kuambata huruma ya Mungu.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Giampietro dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, anakazia kwa namna ya pekee matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huu ni utambulisho na kielelezo cha maisha ya Wakristo; matendo ambayo pengine yalikuwa yamesahaulika katika utume na maisha ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu, anawataka waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu ambayo wakati mwingine imetelekezwa na kupuuzwa. Imani ni kielelezo cha mwamini kukutana na Kristo Yesu katika maisha yake, tayari kumshuhudia kwa watu wanaomzunguka, ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Mungu ni upendo, Deus caritas est!

Askofu mkuu Dal Toso anakaza kusema, matendo ya huruma kiroho na kimwili ni mwaliko wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Matendo haya ni njia makini ya kumwilisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha, kama vile Neno wa Mungu alivyofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake; akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huruma na upendo, ni chanda na pete anasema Mtakatifu Thoma wa Akwino.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.