2016-01-27 08:37:00

Kumekucha! Watawa kuwasha moto wa huruma ya Mungu mjini Vatican!


Mwaka wa Watawa Duniani ambao umekuwa ni hamasa na changamoto kwa Familia ya Mungu kutafakari na kushuhudia matendo makuu ya Mungu kwa mwanadamu unafungwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016, Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia saa 11: 30 jioni kwa saa za Ulaya. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Siku ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, aliwataka watawa wa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, linasema kuanzia tarehe 28 Januari hadi tarehe 2 Februari, 2016, viunga vya Vatican vitawaka moto kwa: Makongamano, Semina na Ibada mbali mbali kama hitimisho la Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Hii ni nafasi muhimu sana kwa watawa wa mashirika mbali mbali kuweza kufahamiana kwa karibu zaidi, tayari kushirikiana kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, maisha ya kitawa ni kielelezo cha umoja unaojidhihirisha pia katika tofauti ya karama na roho za mashirika haya. Hii ndiyo dira itakayoongoza maadhimisho ya kufunga Mwaka wa Watawa Duniani. Tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kumeibuka Mashirika na mifumo mipya ya maisha ya kitawa, kielelezo cha kazi ya Roho Mtakatifu anayeendelea kulitajirisha Kanisa.

Hizi ni siku sita za sala, tafakari, makesha na makongamano, tayari kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa imani na matumaini. Tarehe 28 Januari 2016 kutakuwa na makesha katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 29 Januari 2016, viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume watatoa tafakari kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.