2016-01-26 15:21:00

Rais Hassan Rouhani wa Iran akutana na Papa mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 26 Januari 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Hassan Rouhani, wa Jamhuri ya Kiislam ya Watu wa Iran ambaye baadaye amekutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Galagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo ya viongozi hawa wawili, wamegusia kwa undani tunu msingi za maisha ya kiroho pamoja na kuangalia mahusiano mema ya kidiplomasia kati ya Iran na Vatican; mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Iran, hususan katika kukuza, kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu sanjari na uhuru wa kidini.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamejadili pia kuhusu hitimisho lililofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa kuhusu Mkataba wa Nyuklia; mchango wa Iran katika Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na mataifa mengine huko Mashariki ya Kati, ili hatimaye, amani na maridhiano kati ya watu viweze kudumishwa. Tatizo la mashambulizi ya kigaidi pamoja na biashara haramu ya silaha ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee na Jumuiya ya Kimataifa ili amani na maridhiano yaweze kutawala tena.

Baba Mtakatifu pamoja na Rais Rouhan wa Iran wamekazia pia majadiliano ya kidini, dhamana na wajibu wa dini mbali mbali duniani katika kukuza na kudumisha haki, amani na upatanisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.