2016-01-26 14:13:00

Hija ya Papa Francisko nchini Uswiss ni kukoleza na kudumisha umoja wa Wakristo


Tamko la pamoja kati ya Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo pamoja na Shirikisho la Makanisa la Kiinjili ya Kiluteri Duniani, juu ya ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika Jubilei ya kumbu kumbu ya miaka 500 tangu yalipofanyika mageuzi makubwa ya Kiluteri ndani ya Kanisa, limepokelewa kwa moyo wa shukrani kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo. Tamko hili limekuja wakati, Kanisa linahitimisha Juma la kuombea Umoja wa Wakristo ambalo kwa mwaka huu lilikuwa linaongozwa na kauli mbiu“Mpate kuzitangaza fadhili za Mungu”.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania anasema, maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 500 ya Mageuzi makubwa ndani ya Kanisa linapaswa kuchukuliwa kuwa ni tukio la Kikanisa. Kumbe, Khalifa wa Mtakatifu Petro anayo dhamana na utume wa kuhakikisha kwamba, anajitahidi kuhamasisha, kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na ushuhuda wa umoja wa Wakristo katika: ukweli, sala, upendo na ushuhuda wa damu.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Ruwaichi kwamba, matukio mbali mbali yaliyotekelezwa na Mapapa hususan mara baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican uliokazia kwa namna ya pekee kabisa umuhumu wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo yatawasaidia Wakristo kuona jinsi ya kuendeleza yale wanayopaswa kutenda ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Wakristo.

Iwe ni fursa ya kuangalia mambo yaliyosababisha mpasuko na mgawanyiko wa Kanisa na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, matatizo na changamoto nyingi zimefanyiwa tafakari ya kina na matamko ya pamoja kutolewa. Hatua zote hizi zinaonesha matumaini miongoni mwa Wakristo kwamba, iko siku moja wataweza kuungana pamoja na kuwa wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu.

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, Wakristo wawe na ujasiri wa kutambua makossa na mapungufu yao ya kibinadamu, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu ili kujipatanisha, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa umoja, upendo na ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake. Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo si wakati wa kunyoosheana vidole, bali kwa unyenyekevu kutambua umuhimu wa kutekeleza utashi wa Kristo kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja kama wao walivyo wamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kwa masikitiko makubwa Askofu mkuu Ruwaichi anasema, pale ambapo Wakristo wamekosa kuonesha ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati, wamekuwa ni kikwazo kwa walimwengu. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Lund, nchini Uswiss inalenga pia kukata makali ya kashfa ya utengano miongoni mwa Wakristo, ili wote wawe wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu. Tukio hili linakuja wakati Kanisa Katoliki linaadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto ya kujikita katika toba, wongofu wa ndani, msamaha, haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati, kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.