2016-01-25 07:49:00

Mkwamo wa kisiasa Lesotho: SADC yataka matokeo ya uchunguzi kutangazwa mara moja


Kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika) kimeiagiza Serikali ya Lesotho iwe imetangaza matokeo ya Tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya kisiasa nchini humo ifikapo Februari Mosi, mwaka huu. Agizo hilo lililotolewa kwa Waziri Mkuu wa Lesotho, Dk. Pakalitha Mosisili katika kikao cha SADC Double Troika kilichofanyika mapema wiki hii Gaberone, Botswana, chini ya Mwenyekiti wake, Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama ambaye pia ni Rais wa nchi hiyo.

SADC Double Troika ni kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation) kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana. Pamoja na kutaka Lesotho itangaze matokeo ya tume hiyo, SADC Double Troika iliitaka nchi hiyo iandae mchakato wa kueleza njia za utekelezaji wa mageuzi kama yalivyopendekezwa kwenye ripoti ya tume hiyo ifikapo Agosti, mwaka huu.

“Vilevile, nchi ya Lesotho inatakiwa kuandaa mazingira wezeshi yatakayotoa nafasi kwa viongozi wa upinzani na baadhi ya maofisa wa kijeshi wanaoishi uhamishoni ambao walikimbia machafuko, waweze kurejea nyumbani,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na sekretariati ya SADC siku moja baada ya kikao hicho kumalizika.

Mkutano huo wa Botswana ulihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli; Rais wa Botswana, Luteni Jenerali Khama; Rais wa Afrika Kusini, Bw. Jacob Zuma; Rais wa Msumbiji, Bw. Filipe Jacinto Nyusi; Waziri Mkuu wa Swaziland, Dk. Barnabas Dlamini na Waziri wa Mambo wa Nje wa Zimbabwe, Bw. Simbarashe Mumbengegwi ambaye alimwakilisha Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo.

SADC Double Troika ni mkutano unaohusisha viongozi wakuu watatu wanaoongoza chombo cha ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama na wengine watatu kutoka kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC. Hawa wanawakilisha mwenyekiti aliyepo madarakani, mwenyekiti aliyemaliza muda wake na mwenyekiti ajaye ambaye huwa ni makamu mwenyekiti.

Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Balozi Radhia Msuya, chini ya muundo wa SADC, kuna mambo makuu mawili; la kwanza likiwa ni utangamano wa kikanda ambao unasimamiwa na mkutano wa wakuu wa nchi (SADC Summit) na la pili ni la siasa, ulinzi na usalama ambalo linasimamiwa na chombo maalum (SADC Organ). Akifafanua zaidi, Balozi Msuya alisema wajumbe wa mkutano wa SADC Organ ni Msumbiji (Mwenyekiti); Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda wake) na Tanzania inayotarajia kuchukua uenyekiti wa chombo hiki ifikapo Agosti, 2016. Botswana, Zimbabwe na Swaziland ndizo zinaunda SADC Summit.

Mapema, kikao hicho, kilipokea taarifa ya msuluhishi wa SADC kwenye mgogoro wa Lesotho ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Dk. Cyril Ramaphosa ambayo iliainisha mambo kadhaa yakiwemo ya kikatiba na kiusalama ndani ya nchi hiyo. Dk. Ramaphosa alitakiwa kuhakikisha kuwa mgogoro huo uliovihusisha vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi ya Lesotho, unatatuliwa kwa njia ya mazungumzo kati ya wadau husika ili kuhakikisha kuwa nchi hiyo inarudi kwenye hali ya amani - kisiasa na kiusalama.

Mgogoro wa Lesotho umehusisha kuuawa kwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Lesotho, Luteni. Jenerali Maaparankoe Mahao, mnamo Juni 25, 2015. Pia baadhi ya wananchi wanadaiwa kutiwa vizuizini na wengine kuwekwa ndani.








All the contents on this site are copyrighted ©.