2016-01-23 15:17:00

Waguseni na kuwaburidisha watu kwa Injili ya huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2016 yanaongozwa na kauli mbiu “Mawasiliano na huruma: ni makutano yanayozaa matunda mema”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anawaalika kwa namna ya pekee wadau mbali mbali wa vyombo vya mawasiliano ya jamii kutangaza ukweli unaofumbatwa na huruma ya Mungu; kujenga na kuimarisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana badala ya kuzua kuta za kinzani na mipasuko ya kijamii.

Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii Ijumaa, tarehe 22 Januari 2016 katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko wa Sale, msimamizi wa wadau wa habari, katika mahubiri yake anasema, wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii wanao wito na dhamana kubwa ya kutekeleza ili kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu.

Ibada hii imehudhuriwa na wakuu na wadau mbali mbali wa vyombo vya mawasiliano ya jamii kutoka ndani na nje ya Vatican. Yesu katika maisha na utume wake aliwachagua Mitume kumi na wawili ili kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mitume wakapewa dhamana ya kuhubiri na kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha ya waja wake.

Kumbe, wadau wa vyombo vya upashanaji habari wanapaswa kutambua dhamana na wito wao mbele ya Mungu na jirani zao, ili watu wanaosoma, wanaotazama na kusikiliza matangazo mbali mbali waguswe na huruma na upendo wa Mungu; manukato safi yanayopata chimbuko lake katika Injili ya Kristo. Mtakatifu Francisko wa Sale aliwahi kusema kwamba Injili ni kama Muziki uliotungwa na maisha ya watakatifu ni muziki unaoimbwa na kuburudisha akili na nyoyo za watu!

Vyombo vya upashanaji habari viwaguse na kuwaburudisha watu kwa Injili ya huruma ya Mungu. Ilikutekeleza dhamana hii, wadau wa vyombo vya habari wanapaswa pia kujenga utamaduni wa sala na tafakari, ili kazi na huduma yao, iweze kuwa na manukato ya mambo ya mbinguni, ili kuwatangazia watu Injili ya huruma na matumaini kwa kuwaondolea mambo yanayowasonga na kuwasononesha kama ilivyo kwa Ibilisi.

Wafanyakazi wa vyombo vya habari wawe makini na kile wanachosema, andika na kutangaza. Kwa wafanyakazi wa vyombo vinavyomilikiwa na Kanisa, wanapaswa kulisaidia Kanisa kutoka, ili kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya huruma ya Mungu, ili waweze kuguswa na huruma na upendo wa Kanisa ambalo ni Mama na Mwalimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.