2016-01-23 08:51:00

Utandawazi: Fursa, matatizo na changamoto zilizopo!


Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” Laudato si ni waraka muhimu sana kwa Kanisa ili kuangalia utandawazi: fursa, matatizo na changamoto zake kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa linahamasishwa kufanya upembuzi wa kina kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa; uhusiano kati ya uhuru, Ekolojia sanjari na Ekolojia ya binadamu bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa pia halina budi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuonesha mfano bora wa kuigwa katika misingi ya ukweli na uwazi; tayari kuambata mafao na ustawi na wengi.

Haya ni kati ya mambo msingi yaliyopembuliwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati wa hotuba yake kwa washiriki wa Mkutano wa kimataifa kuhusu utandawazi, ulioandaliwa na Taasisi ya “Acton Institute” Kituo cha tafiti za kidini na uhuru, chenye makao yake makuu nchini Marekani. Mkutano huu uliofanyika hapo tarehe 22 Januari 2016 huko Lisbon, Ureno, umehudhuriwa na Maaskofu 75 waliokuwa wanajinoa kwa mara nyingine tena katika mada ya utandawazi, fursa, matatizo na changamoto zake.

Kardinali Turkson anakaza kusema, Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, una utajiri mkubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote. Hii inatokana na ukweli kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na madhara ya uchafuzi wa mazingira hayabagui wala kuchagua, wote wanaathirika, maskini kwa matajiri. Kumbe, dhamana ya utunzaji bora wa mazingira ni jukumu la watu wote pasi na ubaguzi.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya mazingira na maisha ya binadamu; mambo yanayokamilishana na kutegemezana, changamoto kwa binadamu kuhakikisha kwamba, anatumia vyema nishati rafiki katika mchakato wa uzalishaji na utoaji huduma; changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inapunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo ina madhara makubwa katika maisha na maendeleo ya wengi.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujikita katika ukweli na uwazi kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari kuchukua hatua madhuburi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Wasiwepo wajanja wachache wanaotaka kujitajirisha kutokan ana matatizo na maafa yanayotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kina na wadau mbali mbali: katika ukweli na uwazi ili kuweza kupata matunda yanayokusudiwa na wengi.

Kardinali Peter Turkson anakaza kusema, ulimwengu mamboleo unatawaliwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na fedha; mambo ambayo yanawafanya baadhi ya watu na serikali kuwa na nguvu ya kiuchumi. Lakini, waamini wanapaswa kuendelea kujikita katika sala inayowaonesha kwamba, wanategemea kwa namna ya pekee nguvu ya Mungu, kwa kuonesha upendo na mshikamano pamoja na kuwa na kiasi katika maisha. Yote haya ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha majadiliano na wadau mbali mbali ili kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote, sanjari na kupambana kuna na kupona na umaskini wa hali na kipato, baa la njaa na mardhi.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina ili kutambua na kuthamini kazi ya uumbaji iliyofanywa na Mwenyezi Mungu na baadaye akamkabidhi binadamu aitunze na kuidumisha. Kuna haja ya kuwa na toba na wongofu wa ndani, kwa kuambata sheria na kanuni maadili katika mchakato mzima wa uzalishaji na utoaji huduma kwa jamii. Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano, ili kulinda na kudumisha mafao ya wengi sanjari na kutunza rasilimali ya dunia kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Kardinali Peter Turkson anakaza kusema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanajikita kwa namna ya pekee kabisa katika utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi; mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni; huduma; haki, amani na upatanisho. Haya ni mambo msingi katika kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazotokana na utandawazi pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Binadamu anapaswa kuwa kweli ni rafiki na mtunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.