2016-01-23 07:40:00

Sheria za Kanisa ni kwa ajili ya wokovu wa roho za waamini!


Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wajumbe wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki, “Rota Romana”, Ijumaa tarehe 22 Januari 2016 amesema Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya Mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Kanisa linatambua ndoa kuwa ni kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo!

Ni matumaini ya Monsinyo Pio Vito Pinto Dekano wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki kwamba, sheria mpya iliyopitishwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni kuhusu ndoa zenye utata itatumika kikamilifu, ili kuwapatia waamini chachu mpya ya maisha ya kiroho na kiutu, tayari kuanza upya safari na utume wao ndani ya Kanisa na katika Jamii kwa ujumla wake.

Ndoa na familia ni tunu msingi katika maisha ya binadamu, kama walivyokaza kusema Mababa wa Sinodi ya familia iliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa Kanisa kuwafungulia malango ya huruma ya Mungu wanandoa wanaoogelea katika shida mbali mbali za maisha, ili waweze kupata amani na utulivu mioyoni mwao!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ndiye aliyezindua  Mwaka wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki mjini Vatican kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Paulo mjini Vatican. Katika Ibada hii wamemwomba Roho Mtakatifu awakirimie neema na mapaji ya kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa ajili ya wokovu wa roho za waamini “salus animarum”. Kardinali Parolin amewataka wafanyakazi wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa hekima na busara; kwa kuzingatia haki na mahitaji ya shughuli za kichungaji yanayojikita kwa namna ya pekee katika huruma ya Mungu.

Wafanyakazi hawa wamemwomba Roho Mtakatifu ili aweze kufungua akili na nyoyo zao, ili waweze kufahamu ukweli wa mambo na sheria zilizopo, ili hatimaye, waweze kupata njia muafaka na sahihi inayomwilisha mambo makuu mawili, yaani haki na huruma ya Mungu sanjari na kuzingatia mahitaji ya kichungaji ya kesi wanazoshughulikia, kwani hatima ya mchakato wote huo ni wokovu wa roho za waamini. Ni Roho Mtakatifu peke yake anaweza kuwaongoza wafanyakazi hawa katika ukweli unaozingatia haki na wajibu kwa kufumbatwa na huruma ya Mungu.

Kwa upande wao, Majaji wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki wanapaswa kutenda kwa kuzingatia dhana ya udumifu wa Sakramenti ya Ndoa kwa ajili ya wokovu wa wanandoa wenyewe. Kamwe wasimezwe na mwelekeo na utamaduni wa watu mamboleo wasiotaka kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kisingizio cha uhuru binafsi. Mahakimu wawe mstari wa mbele kukuza, kutangaza na kushuhudia utakatifu na uzuri wa maisha ya ndoa na familia; kwa kuhimiza udumifu na uaminifu; uzazi na malezi ya watoto wao na kwamba, ndoa kati ya Wakristo imepewa hadhi na Kristo mwenyewe kuwa ni Sakramenti Takatifu.

Majaji watambue haki na wajibu, lakini pia wazingatie ukweli na mahangaiko ya watu wa ndoa zenye utata katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Kuna baadhi yao wanaishi na madonda makubwa yanayopaswa kugangwa na kuponywa na huruma ya Mungu, ili kuweza kusonga mbele kwa imani na matumaini mapya. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ziwasaidie kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kardinali Pietro Parolin anahitimisha mahubiri yake kwa kukumbusha kwamba, kila kesi inayowasilishwa kwa Majaji, ishughulikiwe kikamilifu na kupatiwa majibu muafaka mintarafu Sheria za Kanisa, msingi thabiti wa wokovu wa roho za watu! Mahakama kuu ya Rufaa ya Kanisa Katoliki kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, wamefungua rasmi shughuli za Mahakama hii kwa mwaka 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.