2016-01-23 06:49:00

Rais Charles Angelo Savarin akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 22 Januari 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Charles Angelo Savarin wa Jumuiya ya Madola ya Dominican; ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake, wamejadili kuhusu mahusiano mema yaliyopo kati ya nchi hizi mbili pamoja na kukazia umuhimu wa ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na Kanisa Katoliki nchini humo; Kanisa ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi na maendeleo ya watu hususan katika sekta ya elimu na huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Viongozi hawa wamegusia pia masuala ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa kukazia zaidi umuhimu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuongeza jitihada za kimataifa katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa sasa yamekuwa ni chanzo kikuu cha maafa ya watu na mali zao, kisiwani Dominican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.