2016-01-22 09:06:00

Watu wote wa Mungu wanaweza kuoshwa miguu Alhamisi kuu jioni!


Baba Mtakatifu Francisko ameamua kufanya mabadiliko kidogo katika Ibada ya kuosha miguu inayoadhimishwa Alhamisi kuu jioni katika Ibada ya Misa Takatifu, Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja takatifu; akaonesha huduma ya upendo kwa kuwaosha mitume wake miguu. Tangu sasa na kuendelea kati ya Watu wa Mungu wanaoweza kuteuliwa ili kuoshwa miguu ni pamoja na wanawake.

Ufafanuzi huu umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika barua ambayo amemwandikia Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kwa kukazia kwamba, upendo wa kidugu ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Familia yote ya Mungu pasi na ubaguzi. Yesu kwa kuwaosha miguu mitume wake, alionesha sadaka kubwa pasi na kujibakiza kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu na kwamba, upendo wake hauna mipaka.

Baba Mtakatifu anasema, amefikia uamuzi huu baada ya kufanya tafakari ya kina na hivyo tangu sasa viongozi wa Kanisa wanaweza kuwateuwa washiriki wa Ibada ya kuosha miguu kati ya Watu wa Mungu waliopo kwenye eneo husika, si lazima wawe ni wanaume au vijana. Tangu sasa wanawake na wanaume wanaweza kuchaguliwa pasi na ubaguzi wa hali na afya zao. Waamini hawa wanapaswa kuonesha umoja na utofauti unaofumbatwa Watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawafafanulia waamini wao tendo la kuoshwa migu, ili wanaposhiriki katika Ibada hii wawe na mang’amuzi mapana zaidi. Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anakaza kusema, waandaaji wa Ibada ya kuosha migu wanapaswa kutekeleza dhamana hii kwa uangalifu mkubwa, ili washiriki waweze kufaidika na matunda yanayokusudiwa na Mama Kanisa, yaani huduma ya upendo wa kidugu, kama ulivyooneshwa na Kristo mwenyewe, upendo, usiobagua wala kumtenga mtu!

Hii ni amri mpya inayowahimiza Wakristo kusikiliza kwa makini na kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, amekuwa akiadhimisha Ibada hii kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa wafungwa na watu wenye shida zaidi, ili kuwatangazai na kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.