2016-01-22 07:49:00

TAMISEMI wahudumieni watanzania kwa huruma, nidhamu na mapendo!


Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi. “Hapa ndiyo kitovu cha nchi na Watanzania wote macho yao yako huku. Kwa nini? Kwa sababu huduma zinasowagusa za barabara, maji, elimu, zinatokea huku kwa maana ya bajeti na usimamizi,” alisema.

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Januari 21, 2016 wakati akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwenye mkutano uliofanyika ofisi ya TAMISEMI mjini Dodoma. “Wananchi wakilalamikia ukosefu wa hizi huduma chanzo ni hapa. Katika wizara kuna mawaziri lakini wao kule ni wasimamizi wakuu. Ninyi chini yenu kuna mikoa, wilaya, halmashauri, rasimali watu na raslimali fedha za kuwasaidia kufikisha huduma tarajiwa kwa Watanzania walio wengi,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ameitaka ofisi hiyo ihakikishe inaisimamia vizuri mikoa na halmashauri ili Serikali iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa.  Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.

“Hatukubaliani na uzembe kwenye idara na halmashauri za wilaya kwa kuwa hivi sasa Serikali ya Awamu ya Tano inasimamia utumishi uliotukuka na wenye uadilifu hivyo kila mmoja ahakikishe anasimamia vizuri eneo lake,”. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo Watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa Serikali kutambua kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema. "Lazima tujenge moyo wa huruma wa kuwahudumia wenzetu, anapokuja mwananchi msikilize, mhudumie na mwelekeze eneo sahihi ili aweze kupata huduma. Lazima tusimamie na kuona maeneo yote yanafanya kazi kama ilivyokusudiwa, ili kupata matokeo tarajiwa iwe ni wajibu ya kila mmoja kuhakikisha kuwa anatoa usimamizi thabiti katika eneo lake,” alisisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. George Simbachawene alisema TAMISEMI wapo tayari kubadilika na kufanya kazi kama kauli ya Rais John Pombe Magufuli inavyotaka, yaani HAPA KAZI TU. Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Bernard Makali alimpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kusimamia vizuri masuala ya elimu nchini wakati akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya elimu.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, 








All the contents on this site are copyrighted ©.