2016-01-22 15:35:00

Simameni kidete kulinda na kuwasaidia maskini na mazingira!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu pamoja na Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si ni mada ambazo zinaongoza kongamano la kitaifa la wakurugenzi wakuu wa shughuli za kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, wanaokutana kuanzia tarehe 23 hadi 26 Januari 2016, huko Washington DC, Marekani. Kongamano hili linwayashirikisha pia mashirika kumi na sita ya Kanisa Katoliki nchini Marekani yanayojihusisha na utume wa kijamii.

Kongamano hili limeandaliwa na Tume ya Haki, Amani na Maendeleo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani. Wajumbe 500 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hili, ili kujadili kwa kina na mapana changamoto ambazo zimebainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si. Hapa wajumbe wataangalia kwa undani zaidi sababu zinazoendelea kuwatumbukiza watu katika umaskini wa hali na kipato; vita na kinzani za kijamii sehemu mbali mbali za dunia; ukosefu wa misingi ya haki na amani; umuhimu wa Kanisa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mambo yote haya yanajadiliwa ili kuwawezesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Marekani kujitahidi walau kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati matendo ya huruma: kiroho na kimwili, wale wanaohitaji zaidi msaada wao. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani litaendelea kutoa semina maalum kwa watendaji wake wakuu, ili kukabiliana kikamilifu na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa.

Wachungizi wa mambo wanasema, siku hizi ni fursa kwa wajumbe kutoka katika Majimbo mbali mbali nchini Marekani kuweza kufahamiana na kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika masuala mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa. Watapata nafasi kufahamu yale yanayojiri nchini Marekani na kutoka sehemu mbali mbali za dunia mintarafu changamoto za haki, amani, ustawi na maendeleo ya binadamu.

Ni muda wa kusali na kutafakari kwa pamoja matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wao na mwishoni, watarudia tena azma yao ya kusimama kidete ili kuendelea kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kusikia Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.