2016-01-22 14:45:00

Mawasiliano na huruma: ni makutano yanayozaa matunda mema!


Mama Kanisa mwaka 2016 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipoanzisha maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ili kutoa nafasi kwa Kanisa kupembua na kubainisha fursa, matatizo na changamoto zilizopo katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia ya mawasiliano, ili Kanisa nalo liendelee kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wake.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican, Dr. Paolo Ruffini, Mkurugenzi wa Kituo cha TV200 kinachomilikiwa na kuongozwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia pamoja na Professa Marinella Perroni kutoka Taasisi ya Kipapa ya Liturujia, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi, Roma ndio vigogo waliowasilisha Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2016 ambayo kwa mwaka huu sehemu nyingi duniani itaadhimishwa hapo tarehe 8 Mei 2016, Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni. Maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Mawasiliano na huruma: ni makutano yanayozaa matunda mema”.

Monsinyo Edoardo Vigano’ katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni mintarafu Tamko la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu vyombo vya upashanaji habari, uzuri wake; wajibu wa Kanisa, umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili; haki ya upashanaji habari; nyajibu za watu mbali mbali; Kanisa na shughuli za kichungaji kuhusiana na vyombo vya mawasiliano ya jamii; elimu na majiundo makini ya watumiaji wa vyombo vya upashanaji habari.

Siku ya Upashanaji Habari kwa mwaka huu inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Na kwa mara ya kwanza Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican, matunda ya mageuzi yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa inaadhimisha siku ya kwanza ya Upashanaji Habari Ulimwenguni; ulimwengu ambao kwa sasa unatawaliwa na kuratibiwa na teknolojia ya digitali.

Sekretarieti ya Mawasiliano itasimamia na kuratibu vyombo vyote vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, ili kulisaidia Kanisa kutekeleza dhamana na utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa waja wake kwa njia ya mifumo mbali mbali ya mawasiliano ya kijamii. Lengo kuu ni kuwaonesha wanadamu Uso wa huruma ya Mungu ambao ni Kristo Yesu. Huruma ya Mungu ni vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa na kwamba, mawasiliano na huruma ni makutano yanayotegemeana na kukamilishana. Kuna uhusiano mkubwa kati ya ukimya, kusikiliza na neno na kwamba, ukimya ni sehemu ya mawasiliano inayomwezesha mtu kupata mang’amuzi makubwa zaidi. Watu wanahamasishwa kuwa na uwiano mzuri kati ya ukimya, maneno, picha na sauti; mambo yanayounda mawasiliano ya jamii. Ikumbukwe kwamba, watu wana kiu ya kupata ukimya na utulivu wa ndani, ili kuweza kutafakari matendo makuu ya Mungu katika maisha yao na kwamba, huruma ya Mungu iwaguse na kuwaambata maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili huruma hii iweze kuwainua katika utu na heshima yao kama binadamu. Huruma ya Mungu imwilishwe katika mahusiano ya waamini ndani ya Kanisa lenyewe, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Huruma na upendo wa Mungu ni chemchemi ya maisha ya Kikristo na neema ya kuweza kushiriki katika utukufu wa Mungu.

Dr. Paolo Ruffini, Mkurugenzi wa Kituo cha TV200 kinachomilikiwa na kuongozwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema televisheni inaweza kusaidia kuonesha uso wa huruma ya Mungu kwa waja wake, ingawa si rahisi sana kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika televisheni ambazo zinamezwa kwa kiasi kikubwa na fedha za matangazo ya biashara kama njia ya kujitegemea na kujiendesha kibiashara. Lakini Televisheni inaweza kusaidia kujenga na kuimarisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kama ndugu katika umoja na mshikamano.

Televisheni ziwasaidie watu kushirikishana huruma ya Mungu inayofumbatwa katika maisha ya watu ili kujenga madaraja ya majadiliano katika uhuru, ukweli na uwazi. Televisheni iwe ni kwa ajili ya huduma ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mawasiliano yajengeke katika kusikiliza, kuona na kusoma. Huruma ya Mungu inawasaidia wadau katika sekta ya vyombo vya upashanaji habari kuwa huru kuwatangazia walimwengu ukweli wa mambo!

Professa Marinella Perroni kutoka Taasisi ya Kipapa ya Liturujia, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi, Roma kwa upande wake amejikita katika dhana ya huruma ya Mungu kadiri ya Maandiko Matakatifu kwa kuangalia mfano wa Manabii, lakini zaidi kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe aliyejitahidi kuwahabarisha na kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu; kiasi cha kugusa undani wa sakafu ya mioyo yao. Changamoto kubwa kwa watu wa sasa ni kusikiliza kwa makini na kuelewa yale yanayofundishwa.

Professa Marinella anasema, kuna haja ya kuganga na kuponya kumbu kumbu ambazo zimejeruhiwa  katika imani, ili kutambua na kuthamini Fumbo la Umwilisho linaonesha uwepo wa endelevu wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Kanisa linafumbata Fumbo la kusikiliza na fumbo la kufariji. Mawasiliano ya jamii, yaliwezeshe Kanisa kugusa mioyo ya watu kutoka katika undani wao, ili waweze kuambata hekima, ujuzi na maarifa ya maisha yanayobubujika kutoka katika Fumbo la huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.