2016-01-22 15:16:00

Jubilei ya miaka 50 ya mshikamano kati ya Makanisa USA na Amerika ya Kusini


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha mshikamano wa dhati na Kanisa Amerika ya Kusini na Caribeani kwa kuchangia fedha kama kielelezo chao makini cha kushirikishana imani inayomwilishwa katika matendo. Mshikamano huu wa upendo ulianzishwa kunako mwaka 1966 na kwa mwaka huu waamini wanaadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya mshikamano wa Makanisa.

Askofu Eusebio Elizondo, Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani inayoshughulikia mfuko huu anasema, Kanisa Amerika ya Kusini linakabiliwa na changamoto mbali mbali zinazopaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mshikamano wa dhati na waamini wa Makanisa mengine. Kanisa linahitaji rasilimali fedha, ili kuliwezesha kutekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha na utume wake huko Amerika ya Kusini. Linahitaji fedha ili kusaidia majiundo makini ya mihimili ya Uinjilishaji, tayari kumtangaza na kumshujudia Kristo katika  medani mbali mbali za maisha ya waamini, ili kwa pamoja kushuhudia Injili ya furaha na huruma ya Mungu, husani wakati huu, Mama Kanisa anpoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasema, mshikamano huu pamoja na mambo mengine unalenga kusaidia kukoleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili huko Amerika ya Kusini. Katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, mchango huu kutoka kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Marekani, umesaidia kiasi kikubwa katika maboresho ya mipango ya katekesi, majiundo makini sanjari na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa Makanisa haya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linakumbusha kwamba, Mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko aliwapongeza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa kuonesha mshikamano wa upendo na Kanisa Amerika ya Kusini. Hiki ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Makanisa katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Baba Mtakatifu aliendelea kuonesha matumaini kwamba, ushirikiano wa dhati na Kanisa Amerika ya Kusini, utaendelea kuzaa matunda yanayokusudiwa katika maisha ya kiroho na ushuhuda wa Uinjilishaji wa kina, Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.