2016-01-21 15:17:00

Wivu ni dhambi inayouwa watu kwa maneno!


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Agnesi, Bikira na Shahidi, Baba Mtakatifu katika mahubiri yake  kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Siku ya Alhamisi amesema kwamba, wivu na uchochezi ni dhambi inayowamwangamiza mwanadamu kwa njia maneno. Kwa bahati mbaya, dhambi hii pia iko hata katika Jumuiya za Wakristo. Mfalme Sauli alimwonea wivu Daudi baada ya kuwashinda Wafilisti.

Wanawake wakatoka mbio kwenda kumlaki Daudi, huku wakimpongeza na kumshangilia, jambo ambalo lilizua mtima nyongo kwa Mfalme Sauli, akiwaza moyoni mwake kwamba, pengine Daudi angeweza kumsaliti. Mfalme anashawishika hata kufuata ushauri mbaya kutoka kwa mtoto wake, lakini baadaye akajirekebisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, dhambi ya wivu ni mbaya sana katika maisha ya mwanadamu, inakua na kukomaa kama mti mbaya, kiasi cha kuzuia mti mzuri kukua na kukomaa, kiasi hata cha kukosa amani na utulivu wa ndani.

Wivu unampelekea mtu kuonja kifo. Maandiko Matakatifu yanafafanua kwamba, ni kwa njia ya wivu wa Ibilisi, mauti imeingia duniani. Wivu huu bado unaendelea kuchanua na kushamiri kama mti wa Lebanoni hata leo hii miongoni mwa Jumuiya za Kikristo. Wivu unatamani kifo cha jirani; wivu unaua kwa njia ya maneno. Baba Mtakatifu anasema, waamini wenyewe wanaweza kushuhudia jinsi ambavyo wivu unamaliza maisha ya watu kwa kutokana na masengenyo. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kujitafakari moyoni mwake na kuangalia ikiwa kama anaelemewa na wivu, ambao unaweza kuuwa, ili aweze kuupatia tiba kamili.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wivu umekuwa ni chanzo cha mauaji ya kimbari sehemu mbali mbali za dunia, kwani hali ambayo inawafanya baadhi ya watu kukosa furaha kutokana na mafanikio ya jirani zao. Hii ni dhambi mbaya sana. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya kushinda wivu unaowatumbukiza watu katika kifo.

Pontio Pilato katika hukumu yake, alitambua kwamba, Yesu alikuwa ameshitakiwa kutokana na wivu wa wakuu wa makuhani, lakini akashindwa kuwa na ujasiri wa kutoa hukumu ya kweli, akaruhusu Yesu ahukumiwe kifo. Waamini wamwombe Mungu awasaidie kuwa na neema ya kusimamia ukweli na kamwe wasiruhusu kifo kuwafika watu wasiokuwa na hatia. Kila mtu ana dhambi na karama zake, mwaliko kwa kuangalia karama za wengine kwa moyo wa shukrani bila kumezwa na wivu usiokuwa na mashiko wala mvuto, wivu unaosababisha kifo kwa wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.