2016-01-21 11:09:00

Waamini wa dini ya Kiislam Italia wanamkaribisha Papa kutembelea Msikiti wao


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa KitumeĀ  Uso wa huruma, Misericordiae vultus anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali dunia kwani huruma ya Mungu ni fadhila na utajiri unaofumbatwa katika dini mbali mbali dunia. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na daima malango yake ya huruma yako wazi, ili kumsindikiza mwanadamu katika maisha yake.

Majadiliano ya kidini yawasaidie waamini wa dini mbali mbali kufahamiana, kupendana, kuheshimiana na kusaidiana kwa hali na mali kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu na tofauti zao za kidini na kiimani ni hazina kubwa katika maisha ya kiroho. Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kuondokana na kiburi, ukatili, nyanyaso na ubaguzi, ili kujenga umoja na mshikamano kati ya watu; ili kudumisha haki, amani na maridhiano.

Kwa kutambua changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 20 Januari 2016 amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa waamini wa dini ya Kiislam kutoka Italia, waliofika mjini Vatican ili kutoa mwaliko rasmi kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Msikiti mkuu wa Roma. Ujumbe wa viongozi wa dini ya Kiislam nchini Italia uliongozwa na Rayed Khaled, Rais wa waamini wa dini ya Kiislam nchini Italia pamoja na mabalozi kutoka Falme za Kiarabu, Misri na Morocco.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.