2016-01-21 10:38:00

Onesheni na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!


Kardinali Timothy Dolan, Mwenyekiti wa Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani inayojihusisha na Injili ya uhai, katika barua yake ya kichungaji kwa ajili ya maadhimisho ya Miaka 43 tangu Mahakamu kuu ya Marekani ilipopitisha hukumu inayoruuhusu utoaji mimba kisheria, anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kutangaza, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai na upendo, ambao unamwambata kila binadamu pasi na ubaguzi.

Maadhimisho haya yanatanguliwa na mkesha, Alhamisi, tarehe 21 Januari na Ijumaa, tarehe 22 Januari kunafanyika maandamano makubwa kupinga utamaduni wa kifo kwa kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya uhai. Tangu mwaka 1973, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limekuwa likiaanaa makesha na maandamano makubwa kupinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba.

Takwimu zinaonesha kwamba, wananchi wengi nchini Marekani wanapinga sera za utoaji mimba na kwamba, wanapinga pia hukumu iliyotolewa na Mahakama kuu ya kuruhusu kisheria utoaji mimba. Wananchi wengi wanataka kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya uhai kwa kuwapokea, kuwalea na kuwatunza watoto. Wanasema, fedha inayotumika kugharimia mchakato mzima wa utoaji mimba, ingeweza kusaidia kuenzi na kudumisha ya mtoto ambaye hajazaliwa bado.

Mashuhuda wa Injili ya uhai wanapaswa kuwa na mweleo sahihi kuhusu uhai wa binadamu ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa anasema Kardinali Dolan. Kutokana na kampeni kubwa ya vyombo vya habari inaonekana kana kwamba, utoaji mimba ni msaada mkubwa kwa wanawake na wasichana. Wananchi waongozwe na dhamiri nyofu dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kardinali Dolan anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutumia fursa za makesha na maandamano ya kupinga utamaduni wa kifo, ili kushuhudia kwa matendo msimamo wao katika masuala haya ambayo bado yanawagawa wananchi wengi wa Marekani. Maisha ya binadamu ni matakatifu, yanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kuendelezwa. Kwa waamini ambao wameguswa na kutikiswa na utamaduni wa kifo, basi huu ni wakati wao muafaka wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utamaduni na Injili ya uhai.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.