2016-01-20 11:34:00

Wakristo wanaitwa na kutumwa kuzingaza fadhili za Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Siku ya Jumatano, tarehe 20 Januari 2016 wakati huu Wakristo wanaposali pamoja ili kuombea Umoja wa Wakristo, ambao kwa mwaka huu wanaongozwa na kauli mbiu, “Mpate kuzitangaza fadhili za Mungu”, changamoto na mwaliko kwa Wakristo wote kufanya tafakari ya kina kuhusu Sakramenti ya Ubatizo na wajibu wao wa kuambata huruma ya Mungu inayomwilishwa katika sala na matendo ya huruma kwa watu wote bila ubaguzi. Sala na tafakari za kuombea Umoja wa Kanisa zimeandaliwa na Jumuiya ya Wakristo kutoka Lithuania.

Mtakatifu Petro anawahimiza Wakristo kutambua na kuthamini zawadi ya imani waliyoipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowakumbusha kwamba, wao ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu; watu wa milki ya Mungu; ili wapate kuzitangaza fadhili za Mungu. Wakristo wanahamasishwa na Mama Kanisa kutafakari na kushuhudia umoja wao katika Kristo kama Watu wa milki ya Mungu. Wakristo wote wamepyaisha maisha yao katika Kristo Yesu na hivyo ni ndugu wamoja, licha ya tofauti na utengano wao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa njia ya Ubatizo, Wakristo wamepewa dhamana ya kutangaza matendo makuu ya Mungu, ambaye amewatoa gizani na kuwaonesha mwanga wa ajabu. Katika Juma la kuombea umoja wa Wakristo, Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo wote kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kukua na kukomaa katika umoja unaowaunganisha kuliko hata yale mambo yanayowatenganisha. Kwa njia hii, Wakristo wote wanaweza kujibu wito na mwaliko wa kushirikiana na wengine, hususan maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote waweze kuonja huruma ya Mungu na kamwe hasiwepo mtu anayetengwa na huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Uso wa Huruma ya Mungu ni Yesu Kristo mwenyewe; matumaini na amani ya watu wake. Wakristo kwa pamoja wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ili kuwaonjesha Watu wa Mataifa huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani. Wakristo wakite maisha yao katika Sakramenti ya Ubatizo inayowahamasisha kushirikiana na ndugu pamoja na jirani zao wote.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa waamini kutoka Uganda walioshiriki katika Katekesi yake, ambayo imefanyika kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican. Amewatakia wote maadhimisho mema ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; wawe tayari kutubu na kumwongokea Mungu wanapopita kwenye Lango la huruma ya Mungu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Anawaalika vijana kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo na wagonjwa watolee shida na mahangaiko yao kwa ajili ya umoja wa Wakristo. Kwa wanandoa, wajenge ndani mwao upendo unaojikita katika huruma na kujisadaka pasi ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.