2016-01-20 16:10:00

Teknolojia iwe ni kwa ajili ya huduma bora kwa binadamu!


Maendeleo ya sayansi na teknolojia ni upanga wenye makali kuwili; unaomkumbusha mwanadamu uwezo na kipaji cha ugunduzi ambacho amekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Maendeleo haya yamekuwa ni kichoe kikubwa cha maboresho ya hali ya maisha ya watu katika medani mbali mbali. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maendeleo makubwa katika maisha ya mwanadamu, jambo la kumshukuru Mungu. Lakini pia kumekupo na upande mwingine ambao maendeleo ya sayansi na teknolojia yamegubikwa na giza katika maisha ya mwanadamu.

Kuna baadhi ya watu ndani ya jamii wamekuwa na uwezo mkubwa wa kiuchumi kiasi hata cha kuthubutu kutawala na kuwanyanyasa watu wengine ndani ya jamii. Mfano hai ni utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za Kinyuklia. Hapa jambo msingi ni kujiuliza, Je, maendeleo ya sayansi na teknolojia yametoa kipaumbele cha kwanza kwa mwanadamu, ustawi na mafao ya wengi? Hizi ni kati ya changamoto ambazo zimo katika Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Professa Klaus Schwab, mwanzilishi na Rais mtendaji wa Jukwaa la Uchumi Duniani katika mkutano wake unaoendelea huko Davos, Uswiss, uliofunguliwa tarehe 20 na unahitimishwa hapo tarehe 23 Januari 2016. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umewasilishwa kwa Professa Klaus na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anakaza kusema, mapinduzi ya sayansi na teknolojia awamu ya nne yamekuwa pia ni chanzo kikuu cha kupungua kwa idadi ya fursa za kazi duniani, kiasi cha watu wengi kubaki wakiwa wamepigwa na bumbuwazi, ikiwa kweli maendeleo haya ya sayansi na teknolojia yamekuwa ni kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu. Kuna baadhi ya maendeleo yaliyoonekana kuwa ni chachu ya maendeleo katika mchakato wa ukuaji wa viwanda, lakini baadhi ya nishati hizi kama mafuta, ni tishio kubwa kwa ustawi na maendeleo ya binadamu katika ujumla wake. Ni teknolojia inayotishia mazingira, nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia hayakwenda sanjari na maendeleo ya dhamiri nyofu, tunu msingi za maisha ya kiutu na kiroho pamoja na uwajibikaji wa ujumla. Hapa mwanadamu anajikuta akiwa amezungukwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayohatarisha hata maisha yake mwenyewe, kwa ajili ya kujitafutia faida kubwa na utajiri wa haraka haraka.

Hapa kanuni maadili na utu wema, vimewekwa rehani na badala yake maendeleo ya sayansi na teknolojia yamekuwa ni nguvu ya kiuchumi inayotaka kupata faida kubwa kwa kipindi kifupi sanjari na kutanua matamvua yake katika ulimwengu wa utandawazi unaovuka mipaka ya kijiografia, kisiasa na kiuchumi. Teknolojia inakuwa sasa ni kielelezo cha kumiliki, kutawala na kudhibiti, badala ya kusimama kidete kulinda na kutetea mazingira, nyumba ya wote. Teknolojia inakuwa sasa ni mtawala wa dunia anayejitambulisha kuwa ni mtafutaji na mlimbikizaji wa mali na utajiri kupita kiasi. Hali nii inapelekea udhalilishaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ndiyo matokeo ya kukua na kupanuka kwa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; utandawazi unaowabeza na kuwanyanyasa maskini.

Baba Mtakatifu anawakumbusha matajiri wa dunia, kutowasahau wala kuwabeza maskini, bali wawe makini kusikiliza kilio chao, tayari kuwasaidia kwa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu. Mapinduzi ya kitamaduni katika karne ya ishirini na moja yawasaidie walimwengu kutambua na kuthamini maendeleo ya sayansi na teknolojia inayolindwa na kuongozwa na kanuni maadili na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.