2016-01-20 09:07:00

Lindeni raia wanaokwama katika vita na mipasuko ya kijamii!


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea raia wanaojikuta wakiwa katika maeneo ya vita na vurugu, kwani idadi ya wananchi wanaoathirika kutokana na vita inaendelea kuongezeka maradufu sehemu mbali mbali za dunia. Waathirika wakuu ni wanawake, watoto na wazee; pamoja na uwepo wa makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi. Miundo mbinu ya shule, hospitali na barabara inaharibiwa na watu wanaoteseka zaidi ni raia wa kawaida.

Askofu mkuu Auza ameyasema haya Siku ya Jumanne tarehe 19 Januari 2016 wakati alipokuwa anachangia mada kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu umuhimu wa kuwalinda raia kwenye maeneo ya vita. Raia ni waathirika wakubwa wa vita na kinzani za kijamii; mambo ambayo yana athari kubwa katika huduma za afya, elimu, ustawi na maendeleo ya wengi na kwamba, huu ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa kuhusu utu wa mwanadamu. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kuhakikisha kwamba, inachukua hatua madhubuti ili kuwatetea na kuwalinda raia katika migogoro ya kivita.

Wananchi wawe na ujasiri wa kusema wazi wazi unyama na ukatili wanaofanyiwa na askari wakati wa vita na mipasuko ya kijamii na vyombo vya ulinzi na usalama wa raia na mali zao vinapaswa kutekeleza kikamilifu wajibu wake. Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kukomesha vita na kinzani, ili kujenga na kudumisha amani na usalama. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liwachukulie hatua wale wote wanaosababisha vifo, mateso na nyanyaso kwa raia wakati wa vita; jukumu hili litekelezwe kwa kushirikiana na serikali husika na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika kikamilifu. Wananchi walioathirika kwa vita wapewe msaada wa hali na mali na Jumuiya ya Kimataifa.

Kuhusiana na vifo, nyanyaso na dhuluma zinazoendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia, Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anazungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican alisikika akisema kuna mamillioni ya watu yanayoendelea kuomboleza kutokana na vita, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu; ukosefu wa amani na utulivu wa kisiasa; wakimbizi na wahamiaji; bila kusahau mashuhuda wa imani wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao.

Askofu mkuu Auza kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa watu na nchi ambazo zimeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia na kuwahudumia watu wanaoteseka kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wengi wao wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji, ambao kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kukuza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kunahitajika utashi wa kisiasa ili amani iweze kupatikana huko Mashariki ya Kati. Utumiaji wa raia wasiokuwa na hatia kwa misingi ya kivita ni uvunjaji wa haki msingi na utu wa binadamu. Jumuiya ya Kimataifa iwe mstari wa mbele kuonesha wema kama njia ya kupambana na ubaya; kwa kuondokana na sera na utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na kuanza kujikita katika mchakato wa umoja na mshikamano wa dhati; daima kwa kutafuta mafao ya wengi sanjari na kudumisha amani na usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.