2016-01-20 14:55:00

Ekaristi Takatifu ni zawadi ya upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake!


Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini India imekuwa ni fursa kwa waamini nchini India kuweza kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, kwa kumkimbilia Kristo Yesu ambaye ni zawadi kubwa ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu na kwamba, Ekaristi Takatifu ni zawadi ya upendo na huruma ya Kristo kwa waja wake.

Waamini kwa kupokea huruma inayobubujika kutoka kwa Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na upendo unaofumbatwa katika Ekaristi Takatifu, wanakuwa ni vyombo na wajenzi wa huruma na upendo wa Kristo kwa familia ya Mungu nchini India. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India mara baada ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI aliposhiriki katika uzinduzi wa Kongamano la Ekaristi Kitaifa nchini India.

Kardinali Gracias anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wake kwa njia ya video mwanzo kabisa mwa maadhimisho haya. Wajumbe wanakiri kwamba, wameguswa kwa namna ya pekee na maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Kitaifa na kwamba, wanayo changamoto kubwa mbele yao ya kuhakikisha kwamba, wanamwilisha na kuendeleza yale yaliyowagusa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Waamini wamehimizwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tafakari ya Neno la Mungu katika maisha yao sanjari na kushiriki katika Sakramenti za Kanisa hususan, Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho kwani Sakramenti hizi mbili ni pacha, zinasaidiana na kukamilishana, ili kumwezesha mwamini kuwa kweli imara katika imani tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa imekuwa kama ni kipindi cha mafungo ya maisha ya kiroho, yaliyotawaliwa na ukimya, sala, tafakari na ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo.

Mabingwa wa taalimungu kuhusu Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Msamaha waliweza kuwashirikisha wajumbe na hivyo kukata kiu ya hamu ya mioyo yao na huo ukawa ni msingi thabiti wa kuendeleza haya waliyojifunza kwa ajili ya maboresho ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa na jamii inayowazunguka. Wakleri wengi wameguswa na imani thabiti iliyooneshwa na kushuhudiwa na waamini walei katika tafakari zao kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Kwa hakika waamini walei wakipata katekesi makini anasema Kardinali Gracias wanaweza kuwa kweli ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu sanjari na mwendelezo wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Watu wameshuhudia jinsi walivyoonja na kuguswa na uwepo wa endelevu wa Yesu katika Sakramenti zake; lakini wakasikitishwa na athari, nyanyaso na ukatili unaofanywa na wafanya biashara haramu ya binadamu inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wameshuhudia jinsi imani inavyomwilishwa kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, Ibada kwa Bikira Maria na watakatifu wa Mungu. Wamesikitishwa na ubaguzi unaotendwa katika jamii ya wananchi wa India kutokana na matabaka ya watu.

Familia ya Mungu nchini India wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, wameshirikishana utajiri unaofumbatwa katika madhehebu ya Kanisa Katoliki, kiasi kwamba, wengi walijisikia wakijisemea mioyoni mwao, “tujenge vibanda vitatu hapa”. Lakini, kwa sasa familia ya Mungu nchini India inahamasishwa kuendelea kujikita katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa wote wanaowazunguka kielelezo makini cha imani tendaji.

Kwa sasa wajumbe wamepewa dhamana na changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha jirani zao huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu kwa kuhakikisha kwamba, wafungwa magerezani wanapata haki zao msingi; maskini wanatangaziwa Habari Njema ya Wokovu na huruma ya Mungu katika maisha yao; ili wote kwa pamoja waweze kuonja na kuguswa na huruma pamoja na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.