2016-01-19 07:55:00

Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto ya Jumuiya ya Kimataifa!


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni akichangia mada kwenye mkutano kuhusu changamoto ya wakimbizi uliohitishwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, huko Geneva, Uswiss anasema, jibu makini linaloweza kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta hifadhi na usalama Barani Ulaya ni kuhakikisha kwamba, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii huko Libya, Iraq, Somalia Afghanstan na Eritrea inapatiwa ufumbuzi wa kudumu, haki, amani na usalama vinakuzwa na kudumishwa.

Mkutano huu wa siku mbili umefunguliwa Jumatatu, tarehe 18 Januari na unahitimishwa Jumanne, tarehe 19 Januari 2016, kwa kuwashirikisha viongozi wakuu wa nchi mbali mbali kutoka Barani Ulaya pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Lengo ni kutaka kufahamu vyema changamoto inayoikabili Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na wimbi kubwa la wahamiaji na  wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawahamasisha Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba wanashikamana na kushirikiana kwa karibu zaidi. Ili kuratibu na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Katika siku za hivi karibuni, Umoja wa Ulaya inaonekana umeshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika kuratibu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, changamoto inapaswa kumwilishwa katika mshikamano wa upendo; kwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu pamoja na kushirikiana rasilimali watu na nguvu kazi ili kusaidia kuratibu wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ambalo limejitokeza kwa sasa kuwa ni changamoto kubwa kwa nchi mbali mbali za Umoja wa Ulaya kiasi cha baadhi yake kuamua kufunga mipaka yake kwa muda

Dr. Tveit anakaza kusema, lengo la ushirikiano na mashikamano huu unapania kutoa matumaini kwa maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao. Kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaipongeza Ujerumani kwa kufungua mipaka yake ili kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji, uamuzi wa kihistoria kwa Serikali ya Ujerumani. Huu ni utashi wa kisiasa unaopania kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu pamoja na kuendeleza misingi ya waasisi wa Umoja wa Ulaya ambayo inajikita katika: mshikamano, haki, ukweli, uwazi, ukarimu na udugu.

Changamoto ya kusikiliza kilio cha wakimbizi na wahamiaji kimesikika sehemu mbali mbali za dunia kikitolewa na viongozi wa Makanisa, kumbe, viongozi hawa wanapaswa kusikilizwa kwa makini, ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji walau kupata mahitaji msingi pamoja na kuendelea kuwekeza rasilimali ili kuwaingiza wakimbizi na wahamiaji hawa katika mfumo wa maisha ya jamii husika. Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji inapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Mataifa, kila nchi ikijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.