2016-01-19 09:31:00

Vijana wa kizazi kipya wafundwe elimu ya watu kukutana!


Kanisa halina budi kuwasaidia vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kusaidiana, kuheshimiana na kuthaminiana kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hapa binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya elimu makini badala ya kugubikwa na woga pamoja na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko. Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video aliowatumia washiriki wa Kongamano la Ishirini na Nne la Elimu Katoliki Amerika ya Kusini, lililoadhimishwa huko San Paolo del Brasile, hivi karibuni.

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali wa elimu kuhakikisha kwamba, binadamu anapewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kuwafunda vijana katika medani mbali mbali za maisha, ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya maisha yao. Vijana waelimishwe namna ya kufikiri na kutenda vyema katika maisha yao. Haitoshi kuwapatia vijana nadharia ya mambo mengi, bila kugusa undani wa maisha yao. Vijana wafundishwe kutambua mema na kuyatafuta katika maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anatambua na kukiri matatizo pamoja na changamoto ambazo wadau mbali mbali wanakabiliana nazo katika sekta ya elimu; changamoto ambazo zinapaswa kuvaliwa njuga na wahusika, ili kweli elimu inayotolewa iweze kuwa bora zaidi, ili kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kupambana kikamilifu na mazingira yao, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki, amani, umoja na udugu.

Baba Mtakatifu anasema, ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa jamii kujenga na kudumisha utamaduni wa vijana wa kizazi kipya kukutana kati yao, ili waweze kujisikia kuwa ni wamoja; tayari kushirikiana ili kufanya kazi kwa pamoja bila kujali: imani, kabila au mahali anapotoka mtu: hapa utambulisho ni utu na heshima ya binadamu. Kwa njia hii, mchakato wa elimu utawasaidia vijana kukutana na hatimaye, kuzaa matunda yanayokusudiwa na wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mfumo mpya wa shule ujulikanao kama “Scholas occurrentes” unaendelea kushika kasi kwa kujikita katika sana ana michezo; maeneo muhimu sana yanayowakutanisha vijana wa kizazi kipya. Michezo inawasaidia vijana kupata majiundo makini ya kufanya kazi kwa pamoja kwa kutegemeana. Sanaa inawafunda vijana kujenga na kudumisha majadiliano ya kina. Haya ni maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi, ili kweli sekta ya elimu iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Baba Mtakatifu anawataka wadau wa Katoliki kufuata mfano wa Yesu Kristo aliyekuwa ni Mwalimu na Bwana; Mwalimu aliyefaulu kufafanua na kumwilisha Sheria katika uhalisia wa maisha ya watu. Ili waamini waweze kuzama zaidi katika Injili, wanahamasishwa kutafakari, kujisomea na kumwilisha Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake. Matendo ya huruma ni kigezo ambacho Kristo atakitumia wakati atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kumwilisha matendo ya huruma katika maisha ya watu, kielelezo cha imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.