2016-01-19 14:36:00

Kila Mtakatifu ana historia na mapungufu yake!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 19 Januari 2016 amesema kwamba, Mwenyezi Mungu haangalii sura ya nje bali anamwangalia mwanadamu kutoka katika undani wa moyo wake, ndiyo maana akamchagua Daudi kuwa Mfalme wa Israeli. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika maisha ya watakatifu na wenye heri bado kuna vishawishi na dhambi, kumbe hakuna sababu ya kumtumia Mungu kwa ajili ya mafao binafsi.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Mwenyezi Mungu alimkataa Mfalme Saulo kwa sababu alijifungia katika ubinafsi wake, akashindwa kutekeleza mapenzi ya Mungu. Kwa bahati mbaya, binadamu anapenda kuangalia mambo ya nje, lakini Mungu anatambua ukweli unaofumbatwa moyoni mwa mwanadamu. Machoni pa binadamu kijana Daudi hakuwa na thamani kubwa, ikilinganishwa na ndugu zake wengine, lakini huyu ndiye aliyechaguliwa na Mungu ili kuwaongoza watu wake.

Kijana Daudi akapakwa mafuta, lakini katika hija ya maisha yake, akakengeuka na kutenda dhambi, akamwomba Mungu toba na msamaha wa dhambi, akasamehewa dhambi zake. Kutokana na moyo wa toba akajaliwa na Mungu kutenda mambo mengi kwa watu wake, kwa kuwaunganisha. Mfalme Daudi aliteseka kutokana na mapungufu yake ya kibinadamu na daima aliiona wazi dhambi yake mbele yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema hakuna  Mtakatifu asiyekuwa na historia pamoja na mapungufu yake.

Mfalme Daudi angeweza kulipiza kisasi kwa Saulo, lakini hakufanya hivyo, alitubu na kumwongokea Mungu, changamoto kwa kila mwamini kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yake. Kwa njia ya Ubatizo, Wakristo wanafanyika kuwa ni watoto wateule wa Mungu; watakatifu na kwamba, wanahimizwa kutembea katika njia ya utakatifu wa maisha. Kila mtu anayo nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.