2016-01-19 07:08:00

Huruma ya Mungu inaambata maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili!


Huruma ya Mungu ni chachu inayoliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya, pembezoni mwa jamii ili kuwaonjesha watu Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni mwaliko wa kuonesha ukarimu na upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Haya ni mambo msingi ambayo Kanisa linapenda kuyazingatia wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Katika kipindi cha mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu kutafanyika Makongamano makuu mawili: kwanza ni Kongamano la kitume Barani Ulaya, litakaloanza kutimua vumbi mjini Roma kuanzia tarehe 31 Machi hadi tarehe 4 Aprili 2016. Pili Kongamano la kitume kimataifa litaadhimishwa nchini Ufilippini kuanzia tarehe 16- 20 Januari, 2017.

Huu ni ufafanuzi wa kina uliotolewa na Kardinali Christoph Schonborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna ambaye pia ni Rais wa Makongamano ya Kitume Kimataifa alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 18 Januari 2016. Tukio hili limehudhuriwa pia na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji Mpya, Baraza ambalo limepewa dhamana na Baba Mtakatifu Francisko kuratibu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Padre Patrice Chocholski, Katibu mkuu wa Makongamano ya Kitume Kimataifa amehudhuria.

Mazungumzo haya na waandishi wa habari yameratibiwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican. Kardinali Schonborn amefafanua kwamba, Makongamano ya kitume kimataifa, kikanda na kitaifa ni sehemu ya mchakato wa jibu makini linalofumbata tunu msingi za Kiinjili katika kujibu changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kongamano ni dhana ambayo ilipewa kipaumbele cha pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ndio mwendelezo unaofanyiwa kazi hata na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu.

Kanisa linapaswa kutambua kwamba, katika maisha na utume wake linapaswa kuwashirikisha watu huruma ya Mungu. Hii ni changamoto ya pekee kabisa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo wa pili ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu, ndiyo maana hakusita kumtangaza Mtakatifu Faustina Kowalska kuwa ni mtume wa huruma ya Mungu, kama ilivyokuwa kwa watakatifu na wamissionari ambao kweli wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu.

Hawa ni waamini walioingia katika undani na kuonja huruma ya Mungu, kiasi kwamba, wakawa tayari kuishuhudia kwa watu wa mataifa. Huu ni mwaliko wa kuishi na kutembea daima katika huruma na msamaha, huku waamini wakitegemea kwa kiasi kikubwa upendo wa Mungu. Huruma ya Mungu ni kiini cha mafundisho tanzu ya Kanisa; kumbe Wakristo wanahamasishwa kushikamana katika maisha na utume wao, ili kuwaonjesha maskini na wahitaji zaidi huruma na upendo wa Mungu. Hivi ndivyo anavyofafanua Padre Patrice Chocholski, Katibu mkuu wa Makongamano ya Kitume Kimataifa. Huruma ya Mungu ni dhana pana inayojikita hata katika imani ya dini mbali mbali duniani.

Mwenyezi Mungu anatambulikana kama mwingi wa huruma na upole na kwamba, waamini wa dini mbali mbali wanasindikizwa na kutegemezwa katika maisha yao na huruma ya Mungu kama asemavyo Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Uso wa huruma na kwamba, huruma ya Mungu inawaambata wote wanaoikimbilia kwa imani na moyo mnyofu. Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha kukoleza pia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani.

Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inamwambata mwanadamu katika medani mbali mbali za maisha yake, changamoto ya kuonesha ugunduzi, ili kujenga na kudumisha utamaduni mpya wa huruma na mapendo. Makongamano ya Kitume Kimataifa yalifanyika Roma kunako mwaka 2008; Jimbo kuu la Cracovia 2011 na Jimbo kuu la Bogota kunako mwaka 2014. Kongamano la Kitume Kimataifa nchini Ufilippini litakuwa na umuhimu wa pekee kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anasema, maadhimisho ya Kongamano la Kitume Kimataifa Barani Ulaya ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kongamano hili litazinduliwa Jumamosi jioni tarehe 2 Aprili kwa makesha ya sala na kesho yake, Ibada ya Misa takatifu inayotarajiwa kuiongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Hapa lengo ni kukuza na kudumisha tasaufi ya huruma ya Mungu.

Maadhimisho haya yatafuatiwa tena Jubilei kwa ajili ya wafanyakazi na watu wa kujitolea wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili sehemu mbali mbali za dunia. Jubilei hii itaadhimishwa hapo tarehe 4 Septemba 2016. Huruma ya Mungu inagusa na kuambata si tu maisha ya kiroho, bali hali halisi ya maisha ya mwanadamu. Hapa Kanisa pia linapenda kukazia kwa namna ya pekee: toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho. Washiriki wa makongamano haya watapata nafasi ya kushiriki Ibada ya toba ili kujipatia rehema kamili inayotolewa na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.