2016-01-18 08:10:00

Yesu anapenda kukutana na watu katika hali na mazingira yao ya kila siku!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 17 Januari 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekumbusha kwamba, Bikira Maria, Yesu pamoja na wafuasi wake walikuwa wanahudhuria arusi mjini Kana ya Galilaya, na hapo wanaarusi wakatindikiwa divai na Bikira Maria akamjulisha Yesu kwamba, wanaarusi walikuwa hawana divai. Yesu alimjibu mama yake kwamba, saa yake ilikuwa bado haijawadia, lakini akamsikiliza kwa makini na kutenda muujiza wake wa kwanza. Hapo akaonesha utukufu wake na wanafunzi wake wakamwamini.

Baba Mtakatifu anasema, miujiza ni matukio yasiokuwa ya kawaida ambayo yanaambatana na utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuimarisha imani ya wafuasi wa Kristo. Muujiza wa arusi ya Kana ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa wanandoa. Kumbe, upendo wa dhati kati ya bwana na bibi ni njia mahususi ya kuweza kumwilisha Injili, yaani kwa kutembea katika njia inayoelekeza katika utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, muujiza wa Kana unawagusa watu wote wanaoalikwa kukutana na Kristo katika hija ya maisha yao. Imani ya Kikristo ni zawadi ambayo waamini wanaipokea kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowawezesha kukutana na Mwenyezi Mungu. Imani inapitia katika hatua mbali mbali za maisha ya mwanadamu; kuna nyakati za furaha na machungu; kuna nyakati za mwanga na giza kama ilivyo kwa katika mang’amuzi ya upendo wa kweli.

Simulizi la muujiza wa arusi ya Kana linaonesha kwamba, Yesu anapenda kukutana na watu wake katika hali na mazingira yao ya kila siku, na wala si kama Hakimu anayekuja kuwahukumu au Jemedari anayetaka watu wafuate amri na maagizo yake. Yesu anajifunua kama Mkombozi wa binadamu, kama ndugu na kaka mkubwa; Mwana wa Baba wa milele. Yesu anajionesha kama mtu anayetekeleza matumaini na ahadi ambazo zimejichimbia moyoni mwa binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiuliza mioyoni mwao ikiwa kama kweli wanamfahamu fika Kristo na kujisikia kuwa yuko karibu nao na kama wanajibu uwepo wake kwa njia ya mapendo endelevu. Hapa waamini wanahimizwa kutengeneza nafasi mioyoni mwao kwa kutambua kwamba, daima Yesu anatembea pamoja na wafuasi wake.

Katika safari hii ya imani, Yesu amewakirimia wafuasi wake zawadi ya Damu yake azizi. Yale mabarasi yaliyojazwa maji na kugeuka kuwa divai ni alama ya mpito kutoka Agano la Kale kuelekea Agano Jipya. Mahali palipokuwa panatumiwa maji kama alama ya kujitakasa, Yesu anatoa Damu yake Azizi inayomwagika kila siku wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwa namna ya pekee, wakati aliposulubiwa na kuteswa Msalabani. Sakramenti zinazopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka zinawajalia waamini nguvu na neema ya kuonja huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka.

Baba Mtakatifu anahitimisha Tafakari yake kwa kusema kwamba, Bikira Maria ni mfano wa tafakari ya maneno na matendo ya Yesu, awasaidie waamini kugundua ndani mwao uzuri wa imani na utajiri wa Fumbo la Ekaristi Takatifu na Sakramenti nyingine za Kanisa zinaowasaidia waamini kuonja upendo aminifu wa Mungu. Kwa njia hii, waamini wanaweza kuonesha upendo zaidi kwa Yesu Kristo na kumwendea wakiwa na taa za imani yao zinazowaka furaha ili kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya furaha sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.