2016-01-18 10:16:00

Waamini wa dini mbali mbali wakuze misingi ya haki, amani na maridhiano


Viongozi wa Waamini wa dini ya Kiyahudi nchini Italia wamempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kw aujasiri wake katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kweli dini ziweze kuchangia katika ustawi na maendeleo ya jamii husika: kiroho na kimwili; kwa kusimama kidete kupambana na majanga yanayoendelea kumwandama mwanadamu katika maisha, ili kujenga na kudumisha ulimwengu ulio bora zaidi. Baba Mtakatifu ameonesha na kushuhudia urafiki, upendo na mshikamano na waamini wa dini ya Kiyahudi, ili waweze kuheshimiwa na kuthaminiwa badala ya kuwa ni wahanga wa mashambulizi na mauaji kwa misingi ya udini usiokuwa na mashiko wala mvuto.

Ni maneno yaliyotolewa na Ruth Dureghello, Rais wa Waamini wa dini ya Kiyahudi nchini Italia, Jumapili, tarehe 17 Januari 2016 wakati Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Hekalu kuu la waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma. Anakaza kusema, kama waamini wanayo dhamana kubwa mbele yao ya kuhakikisha kwamba, wanasaidia kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Ni wajibu wa waamini kusimama kidete kupinga mauaji ya kimbari.

Imani kamwe haipaswi kuwa ni chanzo cha umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Waamini wa dini mbali mbali wanaalikwa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kwa kujikita katika ukarimu, amani, uhuru, heshima. Waamini wa dini mbali mbali washirikiane na kuwajibikiana, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kwa upande wake, Renzo Gattegna, Rais wa Jumuiya za Kiyahudi nchini Italia katika hotuba yake kwa Baba Mtakatifu Francisko, amepongeza jitihada ambazo zimekwishafikiwa baina ya waamini wa dini hizi mbili katika mchakato wa majadiliano ya kidini katika kukuza na kudumisha uhusiano mwema kati ya Wakatoliki na Wayahudi. Wakatoliki wanatambua umuhimu wa Agano la Kale na imani yake ambayo ni msingi wa Ukristo. Neno la Mungu ni kati ya mambo yanayowaunganisha Wayahudi na Wakristo katika majadiliano ya kidini. Kumbe, waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuheshimu vielekezo vya dini nyingine, ili kujenga na kudumisha haki, amani, uhuru na maridhiano kati ya watu.

Ni jambo lisilokubalika kuona Wayahudi na Wakristo huko Mashariki ya Kati wakiendeleza uadui, chuki, uhasama na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Hii ni changamoto inayoweza kufanyiwa kazi kwa kujikita katika majiundo makini, kwa kuheshimiana na kuthaminiana katika umoja na tofauti zilizopo, kwani huu ni utajiri na hazina muhimu sana kati ya watu sanjari na kukuza tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili zinazowaunganisha kama binadamu!

Wakati huo huo, Rabbi mkuu Riccardo  di Segni, amemwambia Baba Mtakatifu kwamba, Hekalu kuu la Wayahudi mjini Roma ni kielelezo cha uhuru wa kidini baada ya mapambano na nyanyaso za kila aina. Hekalu hili limekuwa ni mahali pa hija pa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia; mahali pa Sala na Ibada. Mbele ya Baba Mtakatifu palikuwepo na mashuhuda walionusurika kwenye mauaji ya kimbari na sasa wamekuwa ni mfano wa kuigwa katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu amewatembelea waamini wa dini ya Kiyahudi, wakati huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, dhana inayopata chimbuko lake katika Biblia. Amri za Mungu, Torah ni msingi thabiti unaotaka kudumisha utu wa binadamu, umoja na uhuru kamili. Jubilei ni kipindi muafaka cha toba, wongofu wa ndani, huruma na mapendo.

Lango la huruma ya Mungu ni kielelezo cha haki na huruma ya Mungu. Waamini wa dini hizi mbili wanayo hazina kubwa inayohifadhiwa mioyoni mwao, lakini mauaji ya kimbari, nyanyaso na dhuluma ni kati ya mambo ambayo yamepelekea kinzani na utengano mkubwa kati ya Wayahudi na Wakristo. Kumbe, kila dini inaweza kukuza na kudumisha Mapokeo yake, ili kujenga amani na kuheshimiana, ushuhuda ambao katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita umetolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa Mstaafu Benedikto XVI na sasa Baba Mtakatifu Francisko.

Rabbi mkuu Riccardo di Segni anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko ni muhimu sana wakati huu, ambapo kuna kilio cha haki, amani, upendo, msamaha na maridhiano kati ya watu kutokana na mauaji yanayofanywa kwa misingi ya udini usiokuwa na mashiko wala mvuto. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika Hekalu kuu la Wayahudi ni mwaliko na changamoto kwa dini mbali mbali kuambata maridhiano, haki na amani. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushirikiana na kushikamana katika masuala mbali mbali ya maisha, ili amani iweze kutawala katika akili na mioyo ya watu. Rabbi mkuu Ricardo di Segni anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufungua malango ya mioyo yao, ili Amri za Mungu ziweze kugusa akili, utashi na uelewa wao, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa malango ya maisha, neema, upendo na huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.