2016-01-18 15:18:00

Papa avishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kudumisha amani na utulivu


Baba Mtakatifu Francisko amevishukuru vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza dhamana na wajibu wake msingi kwa kuzingatia weledi na dhamana kwa maisha ya watu na mali zao. Anatambua na kuthamini uwepo wao wakati wa hija zake za kichungaji sehemu mbali mbali za Italia. Baba Mtakatifu ameyasema hayo, Jumatatu, tarehe 18 Januari 2016 alipokutana na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican ili kutakiana heri na baraka za mwaka mpya wa 2016.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mkutano huu unapewa kipaumbele cha pekee kwani wamekutanika wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tukio muhimu sana katika maisha ya kiroho. Hali hii inajionesha kwa namna ya pekee kwa umati mkubwa wa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaomiminika kila siku mjini Vatican ili kuadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni changamoto kubwa kwa vikosi vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba, maadhimisho haya yanafanyika katika hali ya amani na utulivu. Iwe ni nafasi kwao pia kujenga na kudumisha amani na utulivu wa ndani, wakati  wote wanapotekeleza dhamana na wajibu wao.

Pango la Mtoto Yesu, ni alama ya Fumbo la Umwilisho ambalo Kanisa limeadhimisha hivi karibuni, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kutunza ndani mwao hazina ya imani ya Fumbo la Umwilisho kama alivyofanya Bikira Maria kwa kuwakirimia Mtoto Yesu, chemchemi ya maisha mapya; mfariji wa mioyo ya watu, nuru inayoangaza giza ya mioyo ya binadamu, ili kushinda dhambi. Kwa njia ya Mtoto Yesu, Kanisa limepata fursa ya kutafakari kuhusu Uso wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, katika hija ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Jubilei iwe ni fursa ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani. Baba Mtakatifu anawaalika wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican kuhakikisha kwamba, wanakitumia vyema kipindi hiki cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwamba, anawatakia faraja mioyoni mwao kama ile ambayo wachungaji walioionja pale mjini Bethlehemu. Baba Mtakatifu anawatakia ushirikiano mwema na vikosi mbali mbali vya ulinzi na usalama wanapotekeleza dhamana na wajibu wao, daima wakiomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria, tayari kutembea katika nyayo za Mtoto wake mpendwa, Yesu Kristo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia sala na sadaka yake katika utume wao wa kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.