2016-01-18 08:21:00

Msikubali wajanja wachache wawapokonye matumaini na furaha ya maisha!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 17 Januari 2016 amewakumbusha waamini na mahujaji waliokuwa wamefurika kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya wakimbizi na wahamiaji duniani kwamba, Kanisa lilikuwa linaadhimisha Siku ya102 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2016.

Kwa mwaka huu, Siku hii imekuwa na baraka ya pekee kwani ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wahamiaji na wakimbizi. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wahamiaji na wakimbizi zaidi ya elfu saba kutoka sehemu mbali mbali za Italia waliofika kuadhimisha Siku hii maalum. Amewakumbusha kwamba kila mmoja wao anabeba ndani mwake, historia, utamaduni na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; kwa bahati mbaya wanabeba mioyoni mwao mang’amuzi machungu ya maisha kama vile umaskini, dhuluma, woga na wasi wasi.

Baba Mtakatifu amewaambia kwamba,uwepo wao kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni kielelezo cha matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu. Amewataka kamwe wasikubali watu wachache kuwapokonya matumaini na furaha ya kutaka kuendelea kuishi; mambo ambayo yanabubujika kutoka katika huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaowapokea na kuwakirimia wahamiaji na wakimbizi.

Wahamiaji na wakimbizi mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kabla ya maadhimisho hayo, wakimbizi na wahamiaji walipitia katika Lango la huruma ya Mungu, tukio ambalo limewasaidia kuonja amani ya ndani. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wafungwa wa Gereza la Opera kutoka Milano, Italia walioandaa Hostia ambazo zimetumika wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wakimbizi na wahamiaji.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka watu wote walitikiswa na mashambulizi ya kigaidi nchini Indonesia na Burkina Faso ambako watu 29 walipoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi. Amewaombea wale wote waliopoteza maisha waweze kupata usingizi wa amani nyumbani kwa Baba wa milele pamoja na kusaidia juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa ujenzi wa amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.