2016-01-18 15:33:00

Mpeni nafasi Roho Mtakatifu aweze kuwakirimia ukweli mkamilifu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Siku ya Jumatatu, tarehe 18 Januari 2016 amewataka wakristo kufungua malango ya mioyo yao ili waweze kushangazwa na uwepo wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye waweze kupata utimilifu wa ukweli wote badala ya kuonesha ukaidi na shingo ngumu mbele ya Mwenyezi Mungu, matokeo yake ni kukiona cha mtema kuni kama ilivyokuwa kwa Mfalme Saulo aliyekataliwa mbele ya Mungu kwani alionesha ukahidi na kuabudu miungu!

Kutokana na kuwa na shingo ngumu, Waisraeli wakashindwa vitani na kufunikwa na aibu kubwa, kwani walishikwa na kishawishi cha kutaka kumtolea Mungu sadaka isiyokuwa na sifa, Ibada ambayo waliifanya kwa mazoea. Nabii Samueli anamkaripia Mfalme Saulo kwa kumkumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu anataka kuona utii kwa sauti yake na wala si sadaka.

Huu ndio mwelekeo unaoneshwa na Yesu kwa Mafarisayo wanaowashutumu Mitume wake kwa kutofunga kwa sababu wanaye Bwana arusi, watafunga siku ile atapoondolewa kwao na kwamba, si vyema kuweka kiraka cha nguo mpya kwenye vazi kuu kuu wala divai mpya haiwekwei kwenye viriba vya zamani! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sheria ni kwa ajili ya huduma kwa mwanadamu ambaye pia anapaswa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mwenyezi Mungu. Kwa waamini wenye mioyo wazi kwa Roho Mtakatifu watafanikiwa kupata upya wa maisha na ukweli mkamilifu; kwa kuwa makini katika kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu.

Moyo uliojifunga ndani mwake, hauwezi kupokea mabadiliko. Hii ndiyo iliyokuwa dhambi kubwa iliyotendwa na Mfalme Saulo, kwa kufanya ibada kwa mazoea bila hata ya kusikiliza sauti ya Mungu na matokeo yake wakajikuta wanaabudu miungu wa uwongo na kumsahau Mungu wa kweli. Waamini wawe na ujasiri wa kufungua malango ya mioyo yao, tayari kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao na kwa njia hii wataweza kufahamu na hatimaye, kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Waamini wawe na ujasiri wa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu anakaza kusema Baba Mtakatifu ili aweze kupata ukweli mtimilifu. Wawe huru pasi na kutenda dhambi. Huu ndio ujumbe ambao Mama Kanisa anapenda kuwapatia watoto wake, kwa kuwataka kubadilisha maisha yao, tayari kusoma alama za nyakati kwa kufungua malango ya mioyo yao, ili Roho Mtakatifu aweze kuwapatia fursa ya kufanya mageuzi msingi katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.