2016-01-16 07:11:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu sana katika kipindi cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo Jumapili ya pili ya mwaka C wa Kanisa, Mama Kanisa anatutengea masomo ambayo yanaonesha jinsi gani Mungu anajali haki na furaha ya mwanadamu. Sababu hiyo anakuwa tayari kwa wakati ufaao kumwokoa mwanadamu kutoka kweye magumu, anakuwa tayari kuipigania haki yake. Somo la kwanza tutakalosikia kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya, Mungu anaahidi kuipigania haki ya watu wake Israeli katika kudumisha ufalme, uhuru na furaha yao. Maisha ya furaha watakayokuwa nayo yatafanana na furaha ya kimapendo kati ya bwana na bibi arusi. Mfano huu wa ndoa unaonekana pia katika Injili kama inavyosimuliwa na Yohane, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo anafanya ishara yake ya kwanza ili furaha ya arusi ya Kana iendelee.

Katika somo la pili la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho tunaona jinsi Roho Mtakatifu alivyogawa karama mbali mbali kwa wanadamu, ambazo zinapaswa zitumike kuleta umoja kati ya watu na sio mgawanyo, zilete ustawi na maendeleo ya wengi.

Leo Kanisa linaadhimisha Siku ya 102 ya wakimbizi na wahamiaji duniani, inayoongozwa na kauli mbiu; wahamiaji na wakimbizi wanatuuliza; Jibu la Injili ya huruma. Hawa ni watu wenye utu na heshima zao; wanapaswa kusaidiwa na haki zao kulindwa na kutekelezwa kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Ndugu msikilizaji, Bwana wetu Yesu Kristo anakuwa tayari kufanya ishara ya kugeuza maji kuwa divai ili furaha ya arusi iweze kuendelea. Mvinyo hufurahisha moyo. Hivyo kupungua kwake arusini kulisababisha furaha ya watu kupungua. Hivyo neno la mama yake Maria: hawana divai, linabeba ujumbe ndani yake ya kuwa “hawana furaha”. Kristo anafanya ishara, divai inapatikana ili furaha hiyo iweze kuwepo tena. Divai hii ya sasa anapoionja mkuu wa meza anamuuliza bwana arusi: inakuwaje divai nzuri vile kawapa watu wakielekea mwisho wa sherehe badala ya kuwapa mwanzoni mwa sherehe.

Tunaona hapa ya kuwa furaha inayoletwa na Kristo katika maisha yetu ni furaha ya kimungu, ni furaha nzuri zaidi kuliko furaha tunazojitafutia kwa fikra zetu wenyewe ambazo haziendani na mapenzi ya Mungu. Kuna watu wanaoweza kujiuliza inakuwaje Kristo anaongeza kileo, yaani pombe, arusini. Hapa ni moja ya mahali tunapoalikwa kutafakari vema juu ya furaha ambazo zinakuwa kinyume cha mapenzi ya Mungu. Mwenyezi Mungu alivibariki vitu vyote, hivyo hamkatazi mwanadamu kutumia kileo wala chakula, bali akitumie kadiri ya mahitaji, akitumie kwa kiasi. Kitu chochote kikitumika kwa kuzidisha kipimo kinaumiza. Hivyo wakati furaha ya kibinadamu inaweza kuwa kunywa na kulewa, furaha ya kimungu ni kutumia kileo kiasi kwa afya na kuburudisha moyo, kama tunavyoona katika arusi ya Kana.

Katika arusi hii ya Kana Bwana wetu Yesu Kristo anafanya ishara yake ya kwanza,akaudhihirisha utukufu wake nao wanafunzi wake wakamwamini. Ishara hapa tusitazame ile divai kwa nje tu, tuitizame katika lile lengo, yaani ile nia ya Kristu kwamba: furaha ya mwanadamu arusini na katika ndoa inapaswa iwepo, iendelee na idumu. Hili linawezekana kwa msaada wa Kristu.

Simulizi la Injili linapoonesha kuwa divai imeisha, linaonesha upungufu wa kibinadamu, upungufu ambao kila mmoja anao. Hata katika maisha ya ndoa, wanaunganika watu wawili wenye mapungufu, kila mmoja na udhaifu wake. Kumbe, yanapotokea magumu ama mapungufu hapaswi kukata tamaa, na kwa wana ndoa mapungufu yasiwe sababu ya kukimbia ndoa, sababu za kuomba kuachana, badala yake mkimbilieni Kristo. Ndoa katika Maandiko Matakatifu hutumika pia kama ishara ya muunganiko, umoja na Mungu. Tumesikia hata leo katika kitabu cha Nabii Isaya, Mungu anaonesha furaha ya wana wa Israeli itakavyokuwa kwa mfano wa bwana na bibi arusi, itakuwa kama Mungu anaiposa jumuiya ya waisraeli.

Katika maisha ya ndoa, mnapokutana na magumu mkimbilieni Kristo katika Sala na Sakramenti  za Kanisa; ombeni ushauri kutoka kwa mapadri na watu mbali mbali wanaowazunguka wenye uwezo na busara ya kuwasaidieni. Katika yote hayo, Kristo ndiye awe nguzo yenu, mruhusuni aweze kuwaonesha ishara ya mapungufu na udhaifu wenu; jinsi vinavyoweza kuwa vya msaada kwa ajili ya umoja, upendo na udumifu wenu. Kwa namna hii mtauona utukufu wa Mungu ukijidhihirisha katika ndoa yenu pamoja na udhaifu uliopo.

Ikumbukwe kuwa, Mwenyezi Mungu kampa mwanadamu zawadi ya ndoa na familia tangu kuumbwa kwa Ulimwengu. Mungu anaposema: si vema mtu huyu awe peke yake, ntamfanyia msaidizi wa kufanana naye, kisha anaumba mtu mke, anaonesha hitaji la mwanaume na mwanamke kuishi pamoja na kusaidiana katika ule uhalisia wa kuwa mwanaume na kuhitaji mwanamke na uhalisia wa kuwa mwanamke kuhitaji mwanaume, kukua pamoja na kuutafuta utakatifu kwa maisha ya ndoa. Msaada huu hauishii kwenye uhalisia wa jinsia tu, bali hata uhalisia wa tabia na hali, uhalisia unaoonesha udhaifu wa mmoja unavyoweza kusaidiwa na mwenza wake ili kukua pamoja katika kuutafuta utakatifu. Ndivyo tunavyoona sasa umuhimu wa kuweka karama mbali mbali za kila mmoja ziwe msaada, kwa faida ya mwenza.

Karama mlizonazo ziwafae kudumisha umoja wa ndoa yenu na sio kuwatenganisha, sio kunyanyasana, sio kuoneana kijicho, sio kukomoana na kulipizana visasi, bali ziwe karama zinazowasaidia kudumu katika umoja wa pendo la kimungu mkiongozwa na Roho Mtakatifu.

Karama hizi zinazogawiwa na kufunuliwa kwetu na Roho Mtakatifu, zaweza kuwa za hekima: uwezo wa kupambanua wema na ubaya, nini cha kutenda, namna ya kukitenda, kwa wakati na mazingira stahiki; au karama za maarifa, ambayo ni uwezo wa ufanisi wa shughuli mbali mbali kama udaktari, uchumi, mawasiliano, sayansi, teknolojia, Sanaa na kadhalika.

Karama kama za ushauri, unyenyekevu, usikivu, uvumilivu ziwasaidie katika maisha ya kila siku kukuza mahusiano na ushirikino mbali mbali badala ya kuwagawa. Karama hizi ziwaweke pamoja zaidi ndani ya Kristu, ili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu muweze kushuhudia utukufu wa Mungu unavyotenda kazi ndani yenu ingawa tuna utofauti mbali mbali. Kila mmoja uone karama yako na kuithamini kwa faida ya wengine, na utazame na kuthamini karama za wenzio kwani zinakufaa kwa faida yako kama asemavyo Paolo Mtume: lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.   

Mpendwa msikilizaji nakushukuru sana kwa kuwa pamoja nasi katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu, kwa niaba ya watangazaji wenza wote waliosikika nasema karibu tena juma lijalo katika muda na wakati kama huu. Kutoka Viunga vya Radio Vatican, ni sauti ya kinabii, Padre Celestine Nyanda. 








All the contents on this site are copyrighted ©.