2016-01-16 08:07:00

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ulete mageuzi nchini Nigeria


Askofu mkuu Gabriel Abegurin wa Jimbo kuu la Ibadan Nigeria, anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha ya wananchi wa Nigeria sanjari na kuimarisha zawadi ya imani. Askofu mkuu Abegurin ameyasema hayo hivi karibuni katika mkesha wa Ibada ya Misa Takatifu kwa kuwataka waamini kuwa na mwelekeo chanya zaidi katika maisha yao, badala ya kukatishwa na kujikatia tamaa.

Waamini waendelee kujiimarisha katika imani, utu wema na utakatifu wa maisha, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Waamini wanaweza kuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu ikiwa kama watajitaabisha kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu; pamoja na kuimwilisha imani yao katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Kwa kuwa karibu na Mungu, watapata nafasi ya kuikimbia dhambi n anafasi zake, tayari kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha yao.

Katika ulimwengu mamboleo, chuki, uhasama na hali ya kulipizana kisasi ni mambo yanayoonekana kuwa na nguvu zaidi hata kuliko huruma, upendo na msamaha. Waamini wawe na ujasiri wa kukataa kuvurugwa na vilema vya dhambi yaani: majivuno, uroho, uzinifu, hasira, ulafi, kijicho na uzembe. Waamini wawe tayari kuambata heri za mbinguni na kuanza kutembea katika njia ya utakatifu wa maisha. Hizi ndizo nyenzo muhimu sana zinazoweza kutumiwa na waamini pamoja na wananchi wa Nigeria kubadilisha mfumo wa maisha, kwa mwaka 2016, ili kweli Nigeria na dunia nzima, iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata misingi ya haki, amani, upatanisho na msamaha; kwa kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu, jibu makini kwa watu wanaoteseka na kusononeka katika maisha yao. Wakristo kama walivyo wananchi wengine wa Nigeria, wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao wa kiraia na kikatiba.

Katika mwelekeo kama huu, Askofu mkuu Abegurin anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanasaidia mchakato wa kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali; kwa kujikita katika fadhila za Kikristo, ili kukoleza na kudumisha haki, amani, msamaha na upatanisho mambo muhimu sana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wakristo wakiambatana na Mungu hakuna jambo linaloweza kushindikana kwani Mungu atatenda kwa wakati wake.

Askofu mkuu Gabriel Abegurin anasema, amani, usalama na utulivu kwa mataifa mengi duniani vimetoweka na matokeo yake ni wasi wasi unaoendelea kuijaza akili na mioyo ya watu kutokana na mashambulizi ya kigaidi kama ilivyo nchini Nigeria na sehemu mbali mbali za dunia. Misimamo mikali ya kidini na kiimani, bado imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao. Dhuluma na nyanyaso pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni mambo yanayoendelea kuzalisha makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao.

Kutokana na changamoto hizi, waamini hawana budi kusali pamoja na kutekeleza dhamana na wajibu wao kiraia na kikristo; wakiwa tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, ili kuchangia katika mchakato wa kujenga dunia inayosimikwa katika haki, amani, udugu na mshikamano wa dhati na kwamba, pasiwepo na mtu anatengwa wala kunyanyaswa kutokana na imani au rangi yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.