2016-01-16 10:45:00

Muujiza unajikita katika upendo na ukarimu kwa jirani!


Wapendwa taifa la Mungu, baada ya Adhimisho la sherehe ya Ubatizo wa Bwana, ambapo sisi tumetumwa kushuhudia utukufu wa Mungu na kushiriki katika ujenzi wa huo ufalme, leo tunaona kuwa ili hayo yaonekane au yapate kutendeka hatuna budi kuwajali wengine, ili kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu: wakati wa shida na raha; wakati wa kukata tamaa na kuchanganyikiwa.  

Mwinjili Yohane anasema Yesu anafunua utukufu wake katika tendo la kugeuza maji kuwa divai. Yohani analinganisha tendo hili na ukamilifu wa lengo la ujio wa Kristo: kufunua utukufu wa Mungu. Mwishoni wa Injili yake, Yohane anasema kuwa aliandika neno hilo yaani injili ili watu wapate kuamini. Yoh. 20:20. Mwanzo wa ukamilifu wa lengo hilo ulionekana tayari pale Kana. Yohani anajua wazi kuwa tendo hili la kujifunua lilikamilika pia katika tendo la kujitoa msalabani, pale roho alitolewa. Yoh. 20:22. Tunaona kuwa katika tendo la Kana Yesu anamwambia mama yake saa yangu haijatimia. Saa ya Yesu kadiri ya Yohani ilitimia ule muda kwa kutukuzwa msalabani na katika ufufuko.

Ni saa ambayo amewavuta wote kwake – Yoh. 12:32. Ni ile saa alipotoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba – Yoh. 13:1. Kile kilichofanyika pale Kana kilikuwa ni mwanzo wa kuonekana kwa utukufu wake hadharani. Pale Kana, Yesu alifunua utukufu wake, wafuasi wake walimwamini na Bikira Maria anakuwa mama mshindi dhidi ya shetani.

Kwa namna ya pekee tunaona katika Injili ufunuo wa utukufu wa Mungu. Somo hili laongea kuhusu ukamilifu wa ahadi ya Mungu. Mungu amekamilika katika yote. Na ukamilifu wetu ni kushiriki katika huo mpango wa Mungu wa ukombozi. Mtakatifu Francisko wa Assisi anatambua wazi mpango huu wa Mungu na anatamka wazi akisema ”Ee Mungu unifanye niwe chombo chako cha amani, upendo, huruma, upatanisho n.k.” Mtakatifu huyu anakabidhi maisha yake yote kwa Mungu, ili aweze kuwa kweli ni chombo chake cha huruma na

Mwinjili Yohane anamtaja Maria mara mbili katika Injili yake. Kwanza katika harusi ya Kana na mara ya pili pale chini ya Msalaba Yohane anapenda kuonesha jinsi Mama Bikira Maria alivyoshiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi pamoja na Mwanawe. Neno la Mungu siku ya leo, latupa changamoto juu ya namna ya kushiriki utukufu wa Mungu. Somo la pili toka barua ya mtume Paulo kwa Wakorintho yatosha kuonesha au kutukumbusha kuwa vipaji alivyotujalia Mungu, vyatosha kufanya miujiza. Hatuna budi nasi pia kuangalia matumizi ya vipaji hivyo. Kwanza kila mmoja wetu hana budi kutambua vipaji alivyo navyo na pili kuangalia matumizi yake.

Mtoto mmoja alimwomba baba yake amsimulie hadithi nzuri. Baba yake alikuwa anahangaika sana kuitunza familia yake. Kwa hakika hakuwa na muda wa kukaa na familia yake. Mahangaiko yake yakawa ni kupata chakula n.k ili familia yake ikae vizuri. Huku akidhani kuwa amefanya tendo zuri kwa mwanae, akamnunulia kompyuta nzuri sana na cd nyingi na nzuri zenye hadithi nzuri za watoto. Baada ya muda akaona mtoto wake bado hana furaha. Baba yake akamwuliza kulikoni?. Mtoto akamwambia ni sawa baba, umeninunulia kompyuta nzuri na cd nzuri, lakini wakati nasikiliza hizo hadithi, kompyuta hii haiwezi kunipakata kwa mikono kama ambavyo ungefanya wewe.

Ndugu zangu hatuna budi kujiuliza ni kwa namna gani tunatumia vipaji vyetu na uwezo wetu kwa faida ya wengine. Pengine Neno la Mungu siku ya leo litupe changamoto juu ya namna tunavyotumia vipaji vyetu. Tunaka miiujiza? Basi tuwajali wengine na tuwapatie mambo matakatifu. Hatuna budi kujitoa kwa ajili ya wengine. Na hii itawezekana kama tutakaa na Bwana kama Mama Maria alivyofanya, kuyasikiliza mahitaji na mahangaiko yao na kuyapeleka kwa Yesu. Tukimtumainia Mungu hatutaaibika millele. Somo la kwanza latuambia kuwa ahadi ya Mungu ni kamilifu na timilifu.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yatusaidie kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zetu. Tuwe tayari kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasikiliza na kujibu kilio chao kama sehemu ya umwilishaji wa imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa njia hii Wakristo wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya pale walipoishiwa na “Divai”, Bikira Maria akaguswa na mahangaiko ya wanaharusi hawa, hapo Yesu akatenda muujiza wake wa kwanza.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. R. Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.