2016-01-16 07:29:00

Msiwaangalie watawa kama "nyanya mbichi", hawa ni matajiri wa huruma!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI hivi karibuni, limeadhimisha kongamano la miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwa kukazia umuhimu wa wito wa maisha ya kitawa, changamoto kubwa katika kumwilisha huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu kwa kutambua kwamba, watawa kwa namna ya pekee ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kutokana na maisha na utume wao kwa Kanisa. Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha huruma na mapendo ya Mungu katika vipaumbele vya maisha na utume wao kwa familia ya Mungu.

Watawa wanaweza kutekeleza dhamana na wajibu huu nyeti katika maisha na utume wa Kanisa, ikiwa kama viongozi na walezi katika Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume watatekeleza wajibu wao barabara kwa kuwasaidia vijana kung’amua thamani ya wito na maisha yao katika mchakato wa kumwilisha huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Vijana watambue kwamba, maisha yao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe wanapaswa kuwashirikisha wengine kwa njia ya huduma.

Kongamano la miito mitakatifu kwa mwaka huu wa 2016 limeongozwa na kauli mbiu “Matajiri wa huruma; matajiri wa neema”. Zaidi ya watawa na vijana 650 wameshiriki kikamilifu katika kongamano hili, ambalo pia limehudhuriwa na wakurugenzi wa miito, walezi, na wahudumu katika shughuli za kichungaji kutoka Majimbo mbali mbali nchini Italia.

Monsinyo Nico ‘Dal Molin, Mkurugenzi wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito, kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, kauli mbiu ya Kongamano la miito kwa mwaka 2016 imechukuliwa kutoka kwenye Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya Kuombea Miito Mitakatifu kwa Mwaka 2016, siku ambayo kimsingi itaadhimishwa hapo tarehe 17 Aprili 2016, Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema.

Katika kongamano hili wajumbe wamepembua kwa kina na mapana maudhui, ili kujenga mang’amuzi kuhusu Kanisa ambalo kimsingi ni chombo cha upendo na huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Watawa kwanza kabisa wanajisikia kuwa wamesamehewa; wakaponywa na kupatanishwa na Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha katika miito mbali mbali ndani ya Kanisa.

Huu ndio mwongozo maalum kwa kila mwelekeo wa wito. Shughuli za kichungaji kwa ajili ya kuhamasisha miito hazina budi kujikita katika maisha ya sadaka na majitoleo, ili kuishi na kulitumikia Kanisa linalomwilsiha huruma na upendo wa Mungu kwa watu sehemu mbali mbali za dunia; lakini zaidi kwa njia ya huduma kwa jirani, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.  Watawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa shukrani kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani wamepewa upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Watawa watambue kwamba, Mungu anawapenda, anawalinda na kuwaongoza katika maisha na utume wao, daima wawe ni wepesi kukimbilia ulinzi na tunza yake ya kibaba kwa njia ya: Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na huduma makini inayojikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Monsinyo Nico ‘Dal Molin anasikitika kusema kwamba, watawa wanateseka sana mioyoni mwao, pale wanapoangaliwa kama “nyanya mbichi” au makaburi yaliyosahaulika na watu wanapita juu yake bila kutambua. Mwelekeo na hali kama hii inaweza kusababisha watawa kukata tamaa na matokeo yake ni kujifungia katika undani na ubinafsi wao hata wakati mwingine wanaweza kuchanganyikiwa kabisa! Familia ya Mungu itambue na kuthamini maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa na katika jamii inayowazunguka.

Hawa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, watu wanaojisadaka ili kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma makini katika sekta ya elimu, afya na maendeleo jamii, kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya Mungu! Katika kipindi cha miaka mitatu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limejielekeza zaidi katika mchakato wa utakatifu wa maisha kwa kuangalia uzuri na utakatifu wa maisha ya kitawa; moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutokana na upendo wake wa pekee kwa watawa.

Kwa mwaka 2017, Kanisa nchini Italia litatafakari kuhusu umuhimu na umakini wa tafakari mintarafu mwongozo wa Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Injili ya furaha, “Evangelii gaudium” unaogusia utume na maisha ya Kanisa linalotoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa Watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Kanisa ni Mama na mlinzi wa miito mitakatifu, kumbe, miito inapaswa kuwa na mwelekeo wa Kikanisa zaidi kwa kutambua kwamba, Familia na Jumuiya za waamini zinahamasishwa kuhudumia miito mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa kukoleza utakatifu wa maisha ndani ya Kanisa, tayari kuyatakatifuza hata malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Monsinyo Nico ‘Dal Molin anakaza kusema, miito inahitaji uwepo wa Jumuiya ili iweze kuchipuka, kukua na kukomaa. Dhana hii ni muhimu pale tu miito inapokuwa ni ushuhuda wa sadaka na majitoleo kwa ajili ya Mungu na jirani ndani ya Kanisa la Kristo. Familia na Jumuiya za Kikristo ziwe ni wadau wakuu katika kukuza na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kamwe wasiwe ni vikwazo, kwa njia hii, Kanisa linaweza kuwa na matumaini ya uwepo wa miito mitakatifu hata kwa siku za usoni. Kanisa nchini Italia litaendelea kuwekeza katika miito kwa kufanya tafakari ya kina kuhusu hali halisi, matatizo na changamoto zinazoikabili miito mbali mbali ndani ya Kanisa tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.